Iran yazipongeza Korea 2, yaonya juu ya uchochezi wa US
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepongeza jitihada za viongozi wa Korea Kusini na Korea Kaskazini za kutaka kupunguza taharuki katika Peninsula ya Korea sanjari na kuufanya wa kawaida uhusiano wao uliokuwa umevunjika kwa miongo kadhaa.
Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kukutana viongozi wa Korea hizo mbili ni hatua pevu itakayochangia kuimarisha amani na usalama endelevu sio tu wa eneo bali kote duniani.
Amesema sera ya kudumu ya Iran imekuwa kupinga kuzalishwa, kumiliki, kurundika na kutumia silaha za nyuklia, na ni jambo la kupongezwa kwa nchi hizo mbili jirani kutaka kuona Peninsula ya Korea haina silaha hizo hatari.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, hatua iliyochukuliwa na viongozi hao wa Korea ya kupunguza taharuki na msuguano katika Peninsula ya Korea haipaswi kuandamana na uingiliaji wa masuala ya ndani wa Marekani na uchochezi tarajiwa wa Washington.
Viongozi wa nchi mbalimbali za dunia wameendelea kutangaza uungaji mkono wao kwa mazungumzo ya Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini na Rais Moon Jae-in, Rais wa Korea Kusini yaliyofanyika mapema jana Ijumaa.