Iran: Tutasimama kidete kukabiliana na vikwazo vyovyote vile
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i43788-iran_tutasimama_kidete_kukabiliana_na_vikwazo_vyovyote_vile
Msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, hakuna kikwazo chochote kitakacholenga manufaa ya Jamhuri ya Kiislamu kitakachoachwa vivi hivi hivi bila ya kutumia uwezo wetu wote kupambana nacho.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 28, 2018 23:07 UTC
  • Iran: Tutasimama kidete kukabiliana na vikwazo vyovyote vile

Msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, hakuna kikwazo chochote kitakacholenga manufaa ya Jamhuri ya Kiislamu kitakachoachwa vivi hivi hivi bila ya kutumia uwezo wetu wote kupambana nacho.

Mohammad Bagher Nobakht alisema hayo jana (Jumamosi) kujibu taarifa zinazosema kuwa, nchi za Ulaya zimeiambia Marekani kwamba, kama haitajitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA basi nchi hizo zitaiwekea vikwazo Iran.

Amesema, katika vikao vyao vyote nchi za Ulaya zimekuwa zikisisitiza kuwa zitaendelea kuheshimu kikamilifu mapatano hayo na kwamba haziwezi kuweka tena kikwazo chochote kilichoondolewa au kusimamishwa kwa mujibu wa mapatano ya JCPOA.

Pande zilizofikia mapatano ya nyuklia ya JCPOA

 

Msemaji huyo wa serikali ya Iran aidha amesema, kama nchi za Ulaya zitashirikiana na Marekani kurejesha vikwazo kwa kisingizio cha kuiridhisha Washington ibakie katika mapatano hayo, basi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itachukua hatua zinazofaa kukabiliana na hatua zao hizo.

Mapatano ya nyuklia baina ya Iran na kundi la 5+1 linaloundwa na Uingereza, Ufaransa, Russia, China, Marekani pamoja na Ujerumaini yalianza kutekelezwa mwezi Januari 2016, hata hivyo serikali ya Marekani licha ya kwamba ilikuwa mstari wa mbele kuyafanikisha, imeamua kuyavunja bila ya kuheshimu ahadi zake na wala kuheshimu maamuzi ya nchi nyingine zilizoshiriki katika mapatano hayo ambayo yana baraka kamili za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.