Qassemi: Iwapo Marekani itajitoa katika JCPOA, itapata pigo kubwa
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, iwapo Marekani itajitoa katika mapatano ya nyuklia yanayojulikana kwa kifupi kama JCPOA, basi madhara yake yataikumba Washington yenyewe kabla ya upande mwingine wowote.
Mwandishi wa Radio Tehran amemnukuu Bahram Qassemi akisema hayo leo Jumatatu mbele ya waandishi wa habari wa ndani na nje ya Iran na kuongeza kuwa, mapatano ya JCPOA yana sifa zake za kipekee na si jambo rahisi upande fulani kujitoa vivi hivi tu.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran aidha amesema, tangu alipoingia madarakani rais wa Mrekani Donald Trump hadi hivi sasa amekuwa akizungumzia kujitoa katika mapatano hayo lakini amesema, Iran imetabiri senario na njia zote kuhusu suala hilo na ni jambo lisilo na shaka kwamba Washington itapata pigo kubwa iwapo itajitoa katika JCPOA.
Amesema, ijapokuwa hii si mara ya kwanza kwa Wamarekani kuwaonesha walimwengu kuwa hawaheshimu ahadi zao, lakini iwapo watajitoa katika mapatano hayo, watazidi kudhihirisha uhalisia wao na hakuna nchi yoyote itakayoziamini ahadi za Marekani.
Bahram Qassemi aidha amesema, Iran haitakuwa ya kwanza kuvunja mapatano ya JCPOA lakini vile vile amesema, iwapo katika siku za usoni, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaona mapatano hayo hayana manufaa kwake, wakati huo itachukua uamuzi wa nini la kufanya.
Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekanusha madai ya kufikiwa mapatano mapya baina ya Iran na nchi za Ulaya kuhusiana na JCPOA na kusisitiza kuwa, mazungumzo ya hivi karibuni yaliyofanyika mjini Rome Italia yalikuwa ni muendelezo mazungumzo ya amani ya Munich baina ya Iran na nchi nne za Ulaya kwa ajili ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa Yemen.