Zarif: EU ichukue hatua za kivitendo katika kuendeleza ushirikiano na Iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: "Umoja wa Ulaya unapaswa kuchukua hatua za kivitendo na kuongeza uwekezaji wake nchini Iran katika kuendeleza ushirikiano wa kibiashara na Tehran."
Mohammad Javad Zarif amesema hayo Jumapili hapa Tehran katika mkutano wake na Miguel Arias Canete, Kamishna wa Nishati katika Umoja wa Ulaya. Zarif ameongeza kuwa, tangazo la EU la kufungamana na mapatano ya nyuklia ya Iran yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji (JCPOA) sambamba na hatua tarajiwa ya mashirika makubwa ya Ulaya kusitisha ushirikiano na Iran ni mambo yanayokinzana.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, kujiondoa Marekani katika JCPOA kumepeleka watu wa Umoja wa Ulaya kutaka bara hilo lihifadhi mafanikio ya mapatano hayo ya nyuklia.
Kwa upande wake Kamishna wa Nishati katika Umoja wa Ulaya ameashiria hali ya mapatano ya JCPOA baada ya kujiondoa Marekani na kusema: "Nchi za Ulaya zinalipatia uzito mkubwa suala la kulinda mapatano ya JCPOA na zina irada ya kisiasa ya kutekeleza mapatano hayo sambamba na kuendeleza ushirikiano wa mashirika ya Ulaya na Iran."
Amesema kujiondoa Marekani katika JCPOA kumeziletea nchi za Ulaya matatizo lakini ujumbe wa umoja huo ni kuendeleza ushirikiano na Iran na kulinda mapatano hayo.
Baada ya rais wa Marekani Donald Trump kutangaza Mei 8 kuwa nchi yake imejiondoa katika mapatano ya nyuklia ya Iran, nchi za Umoja wa Ulaya, pamoja na China na Russia zilifanya mkutano na Iran Mei 15 na 16 kuhusu kuendelea kutekelezwa mapatano hayo pasina kuwepo Marekani. Imepangwa kuwa Mei 26 kamati ya pamoja ya JCPOA itakutana Vienna katika ngazi ya wataalamu kujadili mapatano hayo. Kumekuwepo na wasiwasi kuhusu ahadi zinazotolewa na nchi tatu za Ulaya yaani Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kuhusu utekelezwaji wa JCPOA.