Kuendelea vikwazo; kilele cha uadui wa Marekani dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i45240-kuendelea_vikwazo_kilele_cha_uadui_wa_marekani_dhidi_ya_iran
Vikwazo vipya vimetangazwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kufuatia uamuzi wa Marekani wa kujitoa katika makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 31, 2018 20:22 UTC
  • Kuendelea vikwazo; kilele cha uadui wa Marekani dhidi ya Iran

Vikwazo vipya vimetangazwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kufuatia uamuzi wa Marekani wa kujitoa katika makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA.

Siasa za vikwazo za Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran si jambo jipya kwa sababu zimekuwa zikitekelezwa tokea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Baada ya kuchukua uamuzi wa kuitoa nchi yake katika mapatano hayo muhimu ya kimataifa hapo tarehe 8 Mei mwaka huu, Rais Donald Trump wa nchi hiyo alisema kuwa ataanza kutekeleza vikwazo vilivyokuwa vimesimamishwa kwa muda vya nyuklia na vikwazo vingine vipya dhidi ya Iran. Kwa msingi huo, Wizara ya Fedha ya Marekani ilitangaza siku ya Jumatano kuwawekea vikwazo shakhsia kadhaa wa kisiasa na kielimu na vilevile mashirika ya Iran kwa kisingizio cha eti kukiuka haki za binadamu na kubana habari. Kabla ya hapo na mara tu baada ya Marekani kutangaza kujitoa katika mapatano ya JCPOA, wizara hiyo ilimuwekea vikwazo gavana wa benki kuu ya Iran na raia wengine watano wa nchi hii kwa madai ya kujihusisha na mpango wa makombora wa Iran.

Rais Trump wa Marekani aliye na chuki ya kupindukia dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Siasa hizo za vikwazo za Marekani kwa hakika si jambo geni bali zimekuwa zikitekelezwa dhidi ya Iran kwa miaka 40 iliyopita. Lengo kuu la Marekani kutekeleza siasa hizo ni kuushinikiza Mfumo wa Kiislamu wa Iran ili ubadilishe misimamo na sera zake za msingi jambo ambalo halijafua dafu hadi sasa ambapo vikwazo hivyo vimefikia kilele. Katika kipindi hiki chote serikali tofauti za Marekani zimekuwa zikitekeleza vikwazo tofauti ili kuuangusha mfumo wa Kiislamu wa Iran lakini si tu kwamba hazijafikia natija yoyote katika hilo, bali mfumo huu wa Kiislamu umekuwa ukipata nguvu na mafanikio zaidi mbele ya maadui  wake.

Kuhusu suala hilo, hivi karibuni Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akihutubia umati mkubwa wa wanafunzi na walimu kwa mnasaba wa Wiki ya Mwalimu  aliashiria njama ambazo zimekuwa zikifanywa na watawala wa serikai tofauti za Marekani katika kipindi chote cha baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusena: 'Watu wanaotekeleza uadui huu dhidi ya taifa la Iran hivi sasa mifupa yao inaozea chini ya ardhi huku Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiendelea kusimama imara na siku itafika ambapo mwili wa bwana huyu pia (Donald Trump) utazikwa chini ya ardhi, lakini Jamhuri ya Kiislamu bado itaendelea kusimama kwa fahari.' Mwisho wa kunukuu.

Ayatullah Khamenei akizungumza mbele ya jeshi la anga la Iran

Uadui na chuki ya Marekai dhidi ya taifa la Iran inatokana na kusimama imara taifa hili ambalo katika kipindi cha miaka 40 iliyopita limefikia kilele cha fahari na kupiga hatua kubwa za maenedeleo na ustawi katika nyanja tofauti zikiwemo za kielimu, kijeshi na kiulinzi licha ya Marekani kuchukizwa na kupinga jambo hilo kwa nguvu zake zote. Kujiondoa Marekani katika mapatano muhimu ya kimataifa ya JCPOA bila shaka kunatokana na kushindwa nchi hiyo kuzuia maendeleo makubwa ya Iran katika nyanja za teknolojia ya nyuklia, makombora ya kujilinda na ushawishi wa Iran katika eneo la Mashariki ya Kati. Kimsingi watawala wa Marekani wanataka kuifanya Iran iwe kama baadhi ya nchi za Kiarabu ambazo watawala wao ni vibaraka wa moja kwa moja wa nchi hiyo ya Magharibi na kutii amri zake. Kwa maneno ya Kiongozi Muadhamu, Wamarekani wanataka kuwa na vibaraka kama watawala wa baadhi ya nchi za eneo ambao wanatii amri zao bila kusita, lakini Jamhuri ya Kiislamu na taifa la Iran linawadhihirishia wazi heshima na utukufu wake, jambo ambalo wanashindwa kulivumilia.

Nchi zilizoshiriki mazungumzo ya JCPOA

Kwa kuwa na uwezo wake wa ndani ya nchi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imebadilika na kuwa nchi muhimu katika matukio ya kieneo na inaainisha siasa zake za ndani na nje ya nchi kwa msingi na thamani za Mapinduzi ya Kiislamu bila kuzingatia matakwa na maslahi ya watawala wa Marekani. Ni wazi kuwa nguvu na uwezo wa Iran unatokana na uungaji mkono wa wananchi wake, na bila shaka nguvu na uhai unaotokana na uungaji mkono wa aina hiyo hauogopi nguvu yoyote ya kidhahiri ya madola ya kibeberu na yanayotumia mabavu ya Magharibi, yakiongozwa na Marekani. Nguzo hiyo muhimu ya Mapinduzi ya Kiislamu ndiyo inayochochea  uadui na ukhabithi wa Wamarekani dhidi ya taifa hili shupavu la Iran.