Hatua shtukizi na za kivitendo za Iran za kuleta mlingano katika JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i45488-hatua_shtukizi_na_za_kivitendo_za_iran_za_kuleta_mlingano_katika_jcpoa
Uamuzi mpya uliotangazwa na Iran wa kustawisha shughuli zake za nyuklia kufuatia agizo lililotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu umeonyesha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiwezi kutiwa shemere na kuburuzwa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, bali hatamu za kuamua nini la kufanya ziko mikononi mwake.
(last modified 2026-04-29T03:42:39+00:00 )
Jun 06, 2018 09:23 UTC
  • Hatua shtukizi na za kivitendo za Iran za kuleta mlingano katika JCPOA

Uamuzi mpya uliotangazwa na Iran wa kustawisha shughuli zake za nyuklia kufuatia agizo lililotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu umeonyesha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiwezi kutiwa shemere na kuburuzwa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, bali hatamu za kuamua nini la kufanya ziko mikononi mwake.

Ali Akbar Salehi, Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (IAEO) alitangaza jana mbele ya waandishi wa habari kuwa: Mitambo ya umeme ya kiwanda cha Natanz imeshawekwa tayari kwa ajili ya kuzalisha vifaa laki kadhaa mchanganyiko vya aina ya SWU, yaani kifupi cha Separative Work Unit kwa ajili ya kiwanda hicho. Lakini licha ya kuchukuliwa hatua hiyo, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA umetoa taarifa na kueleza kwamba mpango huo uliotangazwa na Iran wa kupanua shughuli zake za nyuklia haujakiuka makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki, Ali Akbar Salehi

Mpango mpya wa shughuli za nyuklia wa Iran ulitangazwa kwenye vyombo vya habari baada ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyed Ali Khamenei kubainisha mwenendo wa kindumakuwili wa nchi za Ulaya kuhusiana na JCPOA. Ayatullah Khamenei aliweka wazi hilo katika hotuba aliyotoa siku ya Jumatatu katika hauli ya mwaka wa 29 tangu alipoaga dunia mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Imam Khomeini (MA), na kutangaza pia kwamba: "Shirika la Nishati ya Atomiki lina wajibu wa kuchukua hatua haraka za utangulizi na za maandalizi yanayohitajika kwa ajili ya kufikia kiwango cha SWU 190,000 , ambapo kwa sasa lifanyike hilo kulingana na makubaliano ya JCPOA."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei akihutubia wananchi katika hauli ya Imam Khomeini (MA)

Kutangulia kuchukua hatua za kivitendo na za kuleta mlingano kulikofanywa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uga wa nyuklia kumeonyesha kuwa kujitoa Marekani kwenye makubaliano ya JCPOA hakuwezi kuliyumbisha taifa hili na kulifanya likubali kuridhia mashinikizo na vikwazo, sambamba na kukubali kupunguza kiwango cha shughuli zake za nyuklia. Hapo kabla pia, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alitoa masharti muhimu kadhaa ya kutekelezwa na nchi za Ulaya ili Iran iendelee kubaki kwenye makubaliano ya JCPOA. Msimamo huo, sambamba na kupanuliwa shughuli za nyuklia kulingana na makubaliano ya JCPOA, kumevuruga mahesabu ya Marekani iliyodhani kwamba itaweza kuibana Iran na kuifanya dhaifu katika kuchukua maamuzi kuhusiana na makubaliano hayo. Nia njema iliyoonyeshwa na Iran kuhusiana na JCPOA, ambayo hadi sasa ingali imefungamana kikamilifu na yale yote iliyojikubalisha kuyatekeleza, haimaanishi kwamba itaendelea kubaki tu kwenye makubaliano hayo yenye ila na kasoro kadhaa sambamba na kuvumilia vikwazo dhidi yake.

Wakala wa IAEA umeshatoa zaidi ya ripoti 10 kuthibitisha kuwa Iran imetekeleza kikamilifu JCPOA

Mehdi Fazaeli, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anayaelezea matukio ya karibuni kuhusiana na JCPOA kwa kusema: "Marekani ilikuwa imepanga kwamba baada ya kujitoa kwenye JCPOA ibaki kuwa na kauli ya mwisho ya kuelekeza mkondo wa makubaliano hayo kivitendo, lakini hotuba ya karibuni ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu makubaliano hayo ya nyuklia na amri aliyotoa ya kuendelezwa shughuli za nyuklia kulingana na JCPOA imeonyesha kuwa Iran haijafunga mikono tu, bali imetumia turufu yake kuupiku upande wa pili."

Kudumu kwa JCPOA bila ya kuwemo Marekani kunategemea sera na misimamo huru ya Umoja wa Ulaya ya kukabiliana na mashinikizo ya Marekani na Israel. Siasa na maneno matupu ya kuunga mkono makubaliano hayo ya nyuklia hazisaidii chochote; na Iran haiwezi kuridhia makubaliano yasiyo na mlingano wenye uzani sawa. Kuhama mashirika ya Ulaya moja baada ya jengine yaliyokuwa yamewekeza hapa nchini kwa kisingizio cha kuhofia vikwazo vya upande mmoja vya Marekani hakuwiyani na siasa za majukwaani za nchi za Ulaya kuwa eti zinapigania kuyalinda makubaliano ya JCPOA.

Iran na nchi zinazounda kundi la 5+1 zilipofikia makubaliano ya nyuklia ya JCPOA

Kwa kuuelewa barabara mwenendo na kauli za baadhi ya nchi za Ulaya za kutaka kuyadumisha makubaliano ya JCPOA sambamba na kuendelezwa vikwazo na kupunguzwa kiwango cha shughuli za nyuklia za Iran, ndipo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akaamuru kupanuliwa shughuli za nyuklia za Iran kwa kusisitiza kuwa, kwa sasa lifanyike hilo kwa kuheshimu makubaliano ya JCPOA. Msimamo huo ni onyo kwa nchi za Ulaya kwamba, kuweza kwa wakati mmoja "kuendeleza JCPOA, kudumisha vikwazo na kuziwekea mipaka shughuli za nyuklia za Iran" ni ndoto ya alinacha ambayo hazitaweza kuifikia katu. Na kuendeleza mwenendo huo kunaweza kuifanya Iran ijitoe kwenye JCPOA na kustawisha kwa kasi shughuli zake za amani za nyuklia na za kisayansi.

Ifahamike wazi kwamba JCPOA si silaha ya kuishinikizia na kuiwekea mipaka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; na hivi sasa baada ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kubainisha wazi kila kitu, uamuzi sasa ni wa nchi za Ulaya wa kuamua kusuka au kunyoa.

Peiman Saadat, balozi wa Iran katika Umoja wa Ulaya ameandika makala kwenye tovuti ya kanali ya televisheni ya Euronews akitanabahisha kuwa: "Makubaliano ya JCPOA yanaweza kuendelea bila kuwepo moja ya nchi wanachama wa kundi la 5+1; lakini bila ya kuwepo Iran hakutakuwa na JCPOA. Kwa hivyo badala ya kusikia kauli tupu za ahadi za nchi za Ulaya, inachohitaji zaidi Iran hivi sasa ni kupewa hakikisho na kudhaminiwa kivitendo maslahi yake ya kiuchumi.".../