Siku ya Kitaifa ya Teknolojia ya Nyuklia; Jitihada za Kujitosheleza
Maadhimisho ya Siku ya Kitaifa ya Teknolojia ya Nyuklia yamefanyika leo katika hafla maalumu iliyodhuhuriwa na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislam ya Iran sambamba na kuzinduliwa mafanikio kadhaa ya nyuklia.
Tarehe 8 Aprili katika kalenda ya Iran ni Siku ya Kitaifa ya Teknolojia ya Nyuklia.
Mwaka huu kutokana na kusadifiana siku hii na Ijumaa, maadhimisho yake yamefanyika leo Alkhamisi kwa kuzindiliwa mafanikio kadhaa ya nyuklia.
Akihutubu katika kikao hicho Rais Rouhani amesema kuwa dunia imetambua rasmi haki za Iran katika uwanja wa nyuklia.
Rais Rouhani ambaye mapema leo amehutubia maonyesho ya mafanikio ya nyuklia ya Iran amesema kuwa, dunia imekiri kwamba miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia nchini Iran inafanyika kwa malengo ya amani na ndiyo maana imeanza kushirikiana na Tehran katika uwanja huo.
Amesema walimwengu wameona kwamba nguvu ya mantiki katika meza ya mazungumzo imeshinda vitisho na mashinikizo na hapana shaka kwamba, mafanikio ya wanadiplomasia wa Iran katika mwaka uliopita katika meza ya mazungumzo ya nyuklia na nchi za kundi la 5+1 ni miongoni mwa matunda muhimu zaidi ya kidiplomasia ya Iran.
Rais Rouhani ametilia mkazo udharura wa kuamiliana na dunia na wakati huo huo kufanya jitihada kubwa za kujitosheleza na kusema kuwa, juhudi za kufikia kiwango cha kujitosheleza zinapaswa kufanyika kwa gharama ya chini na kwa muda mfupi. Amesisitiza kuwa Iran ni nchi inayotetea haki zake na pale inapolazimu itatumia zana laini na ngumu katika kutetea na kulinda haki zake.
Akihutubu pia katika kikao hicho, Ali Akbar Salehi ambaye ni Makamu wa Rais na Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran ameashiria hatua ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kutangaza mwaka huu wa 1395 Hijria Shamsia ubebe kaulimbiu hiyo ya "Uchumi wa Kimuqawama, Hatua na Vitendo," na kusema: "Taifa kubwa la Iran, kwa muda wa takribani miongo minne baada ya ushindi wa Mapinduzi adhimu ya Kiislamu, limepata uzoefu kuwa, baadhi ya madola makubwa duniani daima yamekuwa yakiibua madai ya uongo dhidi ya mfumo wa Kiislamu.
Salehi amesema: "Ni jambo la kusikitisha kuona kuwa katika kipindi cha miaka 12 iliyopita, madola makubwa duniani yametumia vibaya vyombo vya habari kuibua tashwishi na shaka katika fikra za walimwengu kuhusu malengo ya mpango wa nyuklia wa Iran wenye malengo ya amani."
Salehi ameongeza kuwa pamoja na kuwepo njama za maadui pamoja na mashinikizo ya kidhalimu na yaliyo kinyume cha sheria kuzuia harakati ya taifa la Iran, nchi hii imeweza kuchukua hatua za ustawi wa pande zote.
Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran amesema leo weledi wa mambo ya kisiasa na kiuchumi wamefikia natija kuwa ili ustawi upatikane kunahitajika nishati safi na endelevu. Amesema ni kwa kuzingatia uuhimu wa kulinda mazingira ndio Iran ikaanza shughuli zake za kujenga vituo vya kuzalisha umeme wa nyuklia.
Katika Siku ya Kitaifa ya Teknolojia ya Nyuklia Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezindua mafanikio kadhaa mapya ya wasomi wa hapa nchini katika uga wa nyuklia.
Aidha katika hafla hiyo kumezinduliwa vitabu vitatu kuhusu maudhui za nyuklia.
Hali kadhalika, kwa njia ya video, Rais wa Iran amezindua kituo cha nyuklia katika eneo la Anarak mashariki mwa mkoa wa Isfahan eneo la kati mwa Iran.