Kiongozi Muadhamu: Serikali ina uwezo wa kukwamisha njama za Marekani
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, serikali ya taifa hili endapo itachukua hatua za lazima itaweza kuyapatia ufumbuzi matatizo na kusambaratisha njama za Marekani.
Ayatullah Ali Khamenei amesema hayo asubuhi ya leo katika kikao chake na Rais Hassan Rouhani pamoja na baraza lake la maweaziri ambapo ameisifu misimamo imara ya Rais Rouhani alipofanya safari huko Ulaya hivi karibuni na kuongeza kuwa, kuongeza nguvu na uwezo mbele ya maajinabi hususan Wamarekani ni jambo la lazima na jambo hili linapaswa kufanywa kwa wakati, kwa uwazi na bila kusita.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran sambamba na kusisitiza juu ya udharura wa "kutekelezwa mipango kwa nguvu zote kwa kutumia suhula na uwezo wa nchi" ameongeza kuwa, madola ya Ulaya yanapaswa kutoa dhamana ya lazima kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, ingawa haipasi kufungamanisha masuala ya uchumi wa nchi na kuyasimamisha kwa kutegemea makubaliano hayo.
Ayatullah Khamenei amesisitiza pia udharura wa kupanua udiplomasia na mawasiliano na madola mengine na kuongeza kuwa, ukiachia mbali kesi chache kama Marekani, uhusiano wa nchi hii na madola ya Mashariki na Magharibi unapaswa kuimarishwa kadiri iwezekanavyo na kuongezwa harakati za kidiplomasia zilizo na malengo maalum.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema ni jambo la lazima kuandaliwa "Ramani ya Njia ya Uchumi Imara" kwa ajili ya taifa hili na kubainisha kwamba, endapo hilo litafanyika, wananchi na wanaharakti wa masuala ya kiuchumi watafahamu majukumu yao na wataharakisha kuisadia serikali kutokana na kuhisika uthabiti na utulivu.