Spika wa Bunge la Iran: Wamarekani hawatekelezi ahadi
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Wamarekani wakati wa mazungumzo huzungumza vizuri mno, lakini inapofikia wakati wa utekelezaji hawatekelezi hata ahadi moja waliyoahidi.
Dakta Ali Larijani, amesema hayo katika mazungumzo yake hapa mjini Tehran na Ri Yong-ho, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Korea Kaskazini na kusisitiza kwamba, Wamarekani si watu wanaoheshimu na kutekeleza makubaliano.
Spika Larijani ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina historia ya kufanya mazungumzo na Marekani na ahadi pamoja na majukumu ya Washington katika mazungumzo hayo yalikuwa wazi, lakini hakuna wakati ambao dola hilo liliheshimu na kutekeleza ahadi zake.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kwamba, wakati wa mazungumzo utawaona Wamarekani wakizungumza vizuri na hata kutoa ahadi kemkemu huku wakielezea mustakabali mwema, lakini unapowadia wakati wa amali na kutekeleza kivitendo ahadi, hukwepa na kutotekeleza ahadi yoyote ile.
Dakta Larijani amesema pia kuwa, Tehran inakaribisha kwa mikono miwili suala la kuimarishwa zaidi uhusiano kati ya Tehran na Pyongyang.
Kwa upande wake Ri Yong-ho, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Korea Kaskazini amesema ameridhishwa na hatua za kustawishwa uhusiano kati ya nchi yake na Iran na kuthamini misaada ya Tehran kwa nchi yake katika kipindi cha miaka yote hii.