Zarif: Marekani imejitakia yenyewe kutengwa kimataifa baada ya kujitoa katika JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i47476-zarif_marekani_imejitakia_yenyewe_kutengwa_kimataifa_baada_ya_kujitoa_katika_jcpoa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Marekani imejitakia yenyewe kutengwa kimataifa baada ya kujitoa kinyume cha sheria katika mapatano ya nyuklia na Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 16, 2018 03:08 UTC
  • Zarif: Marekani imejitakia yenyewe kutengwa kimataifa baada ya kujitoa katika JCPOA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Marekani imejitakia yenyewe kutengwa kimataifa baada ya kujitoa kinyume cha sheria katika mapatano ya nyuklia na Iran.

Mohammad Javad Zarif alisema hayo jana usiku katika mahojiano maalumu aliyofanyiwa na televisheni ya Press TV na kuongeza kuwa, leo hii, hata waitifaki wa karibu kabisa wa Marekani ukitoa majirani zetu wachache, hawako pamoja tena na Washington.

Ameongeza kuwa, kitendo cha Marekani cha kujitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA kwa yakini kimeifanya nchi hiyo itengwe waziwazi kimataifa. Vile vile amesema, Marekani inajaribu kuendesha vita vya kisaokolojia dhidi ya Iran.

Mapatano ya nyuklia ya JCPOA yalipasishwa mwaka 2015 na wanachama watano wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikiwemo Marekani pamoja na Ujerumaini wakati wa utawala wa Rais Barack Obama huko Marekani.

Pande zilizofikia mapatano ya nyuklia ya JCPOA, Marekani imo ndani kabla haijatia ulimi puani na kujitoa kwenye mapatano hayo

 

Kwa mujibu wa mapatano hayo, Iran iliahidi kuwekea mipaka baadhi ya masuala yake ya nyuklia katika mkabala wa kuondolewa vikwazo vyote vilivyowekwa dhidi yake kutokana na mradi wake huo wa nyuklia.

Hata hivyo mara baada ya kuingia madarakani, rais mpya wa Marekani, Donald Trump alitishia kuitoa nchi yake katika mapatano hayo na baada ya kuakhirisha kidogo na kuzuka mivutano mikubwa, hatimae tarehe 8 Mei mwaka huu alitangaza rasmi kuitoa Marekani kwenye mapatano hayo yenye baraka kamili za kimataifa.

Baada ya hapo ameamua kurejesha vikwazo vyote vilivyoondolewa dhidi ya Iran na kutoa amri nchi zote duniani zifuate amri zake vinginevyo zitawekewa vikwazo na Marekani.

Hata hivyo vitisho hivyo vya Trump vimepuuzwa na hata waitifaki wa karibu kabisa wa Marekani kama vile Uingereza ambayo imetangaza rasmi kuwa itaendelea kuheshimu ahadi zake katika mapatano ya nyuklia na Iran na haiogopeshwi na vikwazo vya Marekani.