Kelele za John Bolton; Iran itasimama kidete na haitatetereka
John Bolton, Mshauri wa Mais wa Marekani katika Usalama wa Taifa akizungumza mwisho wa safari yake ya siku tatu katika utawala wa Kizayuni wa Israel amekariri madai yake dhidi ya Iran na kusema vitisho na vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vitaongezwa ili kuilazimisha Tehran ibadili msimamo wake.
Mshauri huyo wa Usalama wa Taifa katika Ikulu ya White House akizungumza na waandishi habari katika Ubalozi wa Marekani katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Israel alisema Marekani itaongeza mashinikizo dhidi ya Iran na yatakuwa zaidi ya vikwazo vya kiuchumi. Bolton alidai kuwa, kwa ushirikiano na waitifaki wake, Washington itahakikisha uuzaji nje mafuta ghafi ya petroli ya Iran unafika sufuri.
Bolton ambaye kwa dhati yake ni mashuhuri kama mtu aliye dhidi ya Iran anapinga vikali mpango wa nyuklia wa Iran, makombora ya Iran na pia ushawishi chanya na athirifu wa Iran katika eneo. Ni kwa msingi huo ndio akaingia katika timu ya wapambe wa karibu wa rais Trump wa Marekani.
Timu ya kisiasa na kiusalama ya Trump imetajwa kuwa iliyo dhidi ya Iran na ina misimamo hasimu na ya kufurutu ada dhidi ya Tehran.
Lengo kuu la serikali ya Trump ni kuishinikiza Iran kadiri inavyowezekana ili hatimaye kuilazimisha Tehran ifanye mazungumzo na Washington. Trump mwenyewe ameashiria mara kadhaa kuhusu lengo hilo lakini ukweli ni kuwa, katika kipindi cha miaka 40 ya baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Marekani haijawahi kufanikiwa katika njama kama hizo dhidi Iran.
Katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, serikali tofauti za Marekani zimekuwa zikitumia mbinu mbalimbali za kuishinikiza Iran na kuiwekea nchi hii vikwazo vya kiuchumi. Mbinu hizo zimejumuisha vita na njama mbalimbali kwa lengo la kuilazimisha Iran irejee katika mkondo wa kuwa tegemezi. Lakini kutokana na umoja na mshikamano wa wananchi na wakuu wa Iran njama hizo zimekuwa zikigonga mwamba.

Leo serikali ya Trump inafuata nyayo za tawala zilizotangulia za Marekani na tafauti iliyopo ni kuwa serikali yake haina aibu wala udiplomasia katika kubainisha mitazamo yake na inatoa kila aina ya tuhuma dhidi ya Iran.
Kuhusiana na hili, Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu hivi karibuni aliashiria kukosekana murua katika matamshi ya watawala wa hivi sasa wa Marekani na kusema: "Huko nyuma hawakuwa wakizingatia adabu za kisiasa na udiplomasia katika matamshi yao lakini wakuu wa sasa wa Marekani hawana aibu na wanatumia lugha chafu katika mazungumzo yao na dunia kana kwamba wamepokonywa murua kikamilifu."
Serikali ya Trump sambamba na kuishinikiza kiuchumi Iran kwa kushirikiana na utawala wa Kizayuni wa Israel na utawala wa Saudia, inazidisha pia mashinikizo ya kisiasa dhidi ya Iran ili kubadilisha sera za Iran katika eneo la Mashariki ya Kati.
Ili kufikia lengo lao hilo chafu, Wamarekani wanatoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Iran wakitaka kuzishawishi fikra za umma ziunge mkono mpango wao ulio dhidi ya Iran. Mihimili mikuu ya Marekani na waitifaki wake katika tuhuma dhidi ya Iran ni kudai kuwa Tehran inaunga mkono ugaidi, na kuwa eti ina uwepo haribifu katika nchi za Syria na Yemen. Ni wazi kuwa tuhuma hizo ni kinyume kabisa cha uhalisia wa mambo. Hii ni kwa sababu tuhuma kuwa eti Iran inaingilia mambo ya ndani ya Yemen zinatolewa wakati muungano wa kivita wa Saudia ambao umepata idhini ya Marekani kila siku unahusika na mauaji ya umati ya raia na hasa watoto Wayemen. Kwa mfano, hivi karibuni ndege za kivita za muungano huo wa wa Saudia zililidondoshea bomu basi la watoto wa shule na kuua makumi ya watoto kwa umati na oparesheni hiyo ilitekelezwa kwa bomu lililouzwa na Marekani. Mauaji hayo yanaonyesha wazi kuwa Marekani ni mshirika wa jinai za kivita za Saudia dhidi ya Yemen na hilo linafanyika sambamba na kutoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Iran.
Historia imethibitisha kuwa, kila mahala wanakoingia Wamarekani, uwepo huo huwa haribifu na wenye kusababisha ukosefu wa amani. Miongoni mwa sera muhimu za Marekani ni kuunda makundi mbalimbali ya kigaidi na kuyatumia kwa ajili ya kufikia malengo yake haramu. Kuhusiana na hilo, Stephen Walt, mhadhiri wa uhusiano wa kimataifa katika Chuo Kikuu cha Harvard ametoa tathmini kuhusu sera haribifu za Marekani kwa kusema: "Ushawishi wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi umekuwa na taathira hasi. Matokeo ya vita vya Marekani dhidi ya Iraq mwaka 2003 ni kuibuka kundi la kigaidi la ISIS na kusababisha mauaji ya maelfu ya watu."
Walt anasema mgogoro wa sasa wa Yemen ni 'mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu duniani' na uungaji mkono wa Marekani kwa muungano wa Saudia katika vita hivyo ndio chanzo cha kuibuka mgogoro huo.