Zarif akutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Syria mjini Damascus
(last modified Tue, 04 Sep 2018 03:36:16 GMT )
Sep 04, 2018 03:36 UTC
  • Zarif akutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Syria mjini Damascus

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Bashar al-Assad wa Syria mjini Damascus na kubadilishana mawazo kuhusu masuala mbalimbali ya pande mbili na ya kieneo.

Katika mazungumzo hayo, Muhammad Javad Zarif na Bashar al-Assad walisistiza kuhusu udharura wa kustawishwa ushirikiano wa kiuchumi baina ya nchi mbili na kushiriki mashirika ya Kiirani katika ukarabati na ujenzi mpya wa Syria baada ya ushindi wa Muqawama dhidi ya ugaidi.

Viongozi hao wawili aidha wamesisitiza kuwa baada ya ushindi wa Muqawama dhidi ya ugaidi kuna umuhimu wa Iran na Syria kupanua ushirikiano wao katika nyanja mbalimbali hasa ya kiuchumi na mashirika ya Kiirani kuwa na ushiriki amilifu katika awamu ya ujenzi mpya wa Syria.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Rais wa Syria wamezungumza na kubadilishana mawazo pia kuhusu masuala muhimu zaidi ya uhusiano wa pande mbili na wa kieneo pamoja na ulazima wa wakimbizi kurejea makwao.

Waziri Zarif akiwasili uwanja wa ndege wa Damascus hapo jana

Kabla ya mazungumzo yake na rais wa Syria, Dakta Zarif alikutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje Walid Al-Muallim na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Imad Khamis.

Mara baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa kimataifa wa Damascus hapo jana katika safari yake hiyo ya siku moja nchini Syria, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema: baada ya ushindi mzuri iliopata kambi ya Muqawama dhidi ya makundi kigaidi na yenye misimamo ya kufurutu mpaka nchini Syria, wakati umewadia wa kuijenga upya nchi hiyo; na nchi waitifaki wa kistratejia wa Damascus zina nafasi na mchango katika suala hilo.../