Sep 07, 2018 15:07 UTC
  • Taarifa ya pamoja ya marais wa Iran, Russia na Uturuki kuhusu Syria katika kikao cha Tehran

Marais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Russia, na Uturuki wametoa taarifa ya pamoja baada ya mkutano wao wa pande tatu mjini Tehran ambapo wamesisitiza kuhusu msimamo wao wa kudumishwa uhuru, mamlaka ya kujitawala na kulinda mipaka yote ya Syria.

Marais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Vladimir Putin wa Russia, na Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki katika taarifa yao ya mwisho leo Ijumaa wamabainisha azma yao ya kuendelea kushirikiana kuangamiza makund ya kigaidi ya ISIS au Daesh, Jabhatun Nusra na makundi mengine ya kigaidi yakiwemo yale yenye mfungamano na al Qaeda au ISIS nchini Syria.

Taarifa hiyo iliyokuwa na vipengee 12 imesisitiza kuwa mgogoro wa Syria hauna suluhisho la kijeshi nakwamba  njia pekee ya kumaliza mgogoro huo ni mchakato wa kisiasa na mazungumzo.

Marais wa Iran, Russia na Uturuki wamebaiisha hamu na nia yao ya kweli ya kuendelea kushirikiana kusogeza mbele mchakato wa kisiasa unaokwenda sambamba na Kongamano la Kitaifa la Mazungumzo ya Syria ambalo lililofanyika mjini Sochi Russia na pia kwa mujibu wa Azimio 2254 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Marais wa Iran, Russia na Syria pia wamesisitizia nia yao ya kweli ya kuendeleza jitihada za pamoja za kutafuta suluhisho la kudumu la kisiasa la mgogoro wa Syria.

Mkutano wa pande tatu wa marais wa Iran, Russia na Uturuki kuhusu Syria

Viongozi hao watatu wamesema kuwa, wataunga mkono hitihada zote za kurejesha maisha ya kawaida Syria na wametoa mwito kwa jamii ya kimataifa hasa Umoja wa Mataifa uipe misaada ya kibinadamu Syria kama ambavyo wametoa mwito wa kuwepo mazingira bora ya kurejea wakimbizi Wasyria katika nchi yao na kuimarishwa miundombinu ya nchi hiyo.

Katika hotuba yake aliyoitoa mapema leo kwenye mkutano huo, Rais Hassan Rouhani amesisitiza kuwa Marekani iko kinyume cha sheria nchini Syria na inazidi kuchochea mgogoro katika nchi hiyo na ameitaka iondoke nchini humo mara moja. Kwa upande wake Rais Putin amesema kuondolewa magaidi katika eneo la Idlib ndicho kipaumbele muhimu cha mchakato wa amani wa Syria hivi sasa.

Aidha amesema Russia ina ushahidi kuwa magaidi wana nia ya kufanya hujuma ya kemikali za sumu katika eneo hilo. Magaidi hufanya hujuma kama hizo ili serikali ya Syria ilaumiwe na kudaiwa kuwa ndiyo iliyohusika. Rais Putin aidha ameelezea matumaini yake kuwa magaidi watakuwa na busara na wataweka chini silaha. Kwa upande wake, Rais Erdogan wa Uturuki katika hotuba yake ameelezea matumaini yake kuwa mkutano wa Tehran utatoa mchango mkubwa katika kupatikana amani ya kudumu Syria.

Tags