Sep 22, 2018 03:12 UTC
  • Iran yakanusha madai ya kuomba kufanya mazungumzo na Trump

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyataja kama kichekesho madai kwamba taifa hili limeomba kufanya mkutano na Rais Donald Trump wa Marekani.

Bahram Qassemi aliyasema hayo jana Ijumaa katika mahojiano na shirika la habari la IRNA na kubainisha kwamba,  madai ya baadhi ya vyombo vya habari kwamba vimemnukuu Nikki Haley, Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa akisema kuwa Rais Hassan Rouhani wa Iran ameomba kufanya mkutano wa pande mbili kati yake na Trump, hayana msingi.

Amesema madai hayo ni sehemu ya propaganda za vyombo vya habari ya kujaribu kupotosha uhalisia wa mambo na kuzihadaa fikra za walio wengi.

Qassemi amesema taifa hili halioni umuhimu wa kufanya mazungumzo na nchi ambayo haiheshimu mapatano ya kimataifa kama vile makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Trump aliiondoa US katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, nchi hii haijawahi hata siku moja, kuomba kufanya mkutano wa pande mbili na Marekan.

Amefafanua kwamba, katika siku chache zijazo, Rais Rouhani ataelekea New York kwa ajili ya kushiriki mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, na wala hana mpango wowote wa kukutana na Trump ambaye ataongoza mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Tags