Iran na Afrika Kusini kuimarisha ushirikiano wa kiulinzi
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Afrika Kusini zimesisitiza juu ya azma zilionayo ya kuimarisha ushirikiano wa kiulinzi baina yao.
Hayo yamebainika kufuatia kikao cha pili cha Kamisheni ya Pamoja ya Ushirikiano wa Kiulinzi kati ya Iran na Afrika Kusini kilichofanyika mjini Pretoria Afrika Kusini.
Mkutano wa pili wa Kamisheni ya Pamoja ya Ushirikiano wa Kiulinzi kati ya Iran na Afrika Kusini ulioanza tarehe 9 mwezi huu ulimalizika jana mjini Pretoria.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Brigedia Jernerali Muhammad Ahadi, Naibu Waziri wa Ulinzi wa Iran katika masuala ya kimataifa na Sam Gulube Katibu wa Kudumu wa Wizara ya Ulinzi ya Afrika Kusini.
Pande mbili katika mkutano huo zimesisitiza juu ya kuimarishwa na kustawishwa zaidi uhusiano wa pande mbili katika masuala ya kiulinzi sambamba na kubadilishana taarifa na tajiriba katika uwanja huo.
Aidha Kamisheni ya Pamoja ya Ushirikiano wa Kiulinzi kati ya Iran na Afrika Kusini imetaka kuweko ushirikiano wa kiuchunguzi na utoaji mafunzo baina ya pande mbili hizo.
Kadhalika mkutano wa Kamisheni ya Pamoja ya Ushirikiano wa Kiulinzi kati ya Iran na Afrika Kusini umejadili njia za kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande mbili.
Vilevile pande mbili zimetiliana saini mwishoni mwa mkutano huo, hati za vipengee vya ushirikiano vilivyofikiwa katika mkutano wa pili wa Kamisheni ya Pamoja ya Ushirikiano wa Kiulinzi kati ya Iran na Afrika Kusini.