Zarif: Vikwazo vipya vya US dhidi ya Iran vinakiuka maamuzi ya ICJ
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i48882-zarif_vikwazo_vipya_vya_us_dhidi_ya_iran_vinakiuka_maamuzi_ya_icj
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Marekani imekubuhu na ni mraibu mkubwa wa kuyawekea mataifa mengine vikwazo, na kwamba vikwazo vipya dhidi ya Tehran ni ukiukaji wa moja kwa moja kwa maamuzi ya hivi karibuni ya Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 18, 2018 10:34 UTC
  • Zarif: Vikwazo vipya vya US dhidi ya Iran vinakiuka maamuzi ya ICJ

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Marekani imekubuhu na ni mraibu mkubwa wa kuyawekea mataifa mengine vikwazo, na kwamba vikwazo vipya dhidi ya Tehran ni ukiukaji wa moja kwa moja kwa maamuzi ya hivi karibuni ya Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ).

Katika ujumbe alioutuma kwenye ukurasa wake wa Twitter, Mohammad Javad Zarif amesema, "Uhasama wa Marekani dhidi ya taifa la Iran umeifanya nchi hiyo iwe mraibu wa kuwekeana vikwazo kinyume cha sheria za kimataifa. Uraibu huo sasa umevuka mipaka."

Zarif ameongeza kuwa, hatua ya Marekani ya kutangaza vikwazo vipya dhidi ya taasisi kadhaa za Kiirani mbali na kukiuka uamuzi wa hivi karibuni wa ICJ, lakini pia ni upuuzaji wa wazi wa mfumo wa sheria na ukiukaji wa haki za binadamu.

Hapo jana Wizara ya Hazina ya Marekani iliyawekea vikwazo mashirika kadhaa ya Iran zikiwemo benki 20, kwa kisingizio cha kuwa na ushirikiano na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) na eti kwa ajili ya kupambana na ugaidi.

Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu ICJ hivi karibuni iliitaka US kuifutia Iran vikwazo

Mahakama hiyo ya ICJ yenye makao yake The Hague, Uholanzi siku chache zilizopita ilitangaza hukumu yake kuhusu kesi iliyofunguliwa na Iran mwezi Julai mwaka huu dhidi ya Marekani, ambapo Tehran iliitaka mahakama hiyo iilazimishe Marekani isimamishe vikwazo vyake vya upande mmoja dhidi ya Iran baada ya Washington kujitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA mwezi Mei mwaka huu.

Mahakama hiyo iliiamuru Washington kusimamisha vikwazo vyake vya upande mmoja haraka iwezekanavyo dhidi ya Iran. Hata hivyo Washington ilisema uamuzi huo wa majaji wa ICJ hauna itibari na wala haitaufuata.