Iran yaitaka dunia iheshimu uamuzi wa ICJ dhidi ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i49054-iran_yaitaka_dunia_iheshimu_uamuzi_wa_icj_dhidi_ya_marekani
Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amezitaka nchi zote huru duniani kufungamana na uamuzi wa hivi karibuni wa Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ), kwa kutouinga mkono Marekani kuiwekea vikwazo Tehran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 26, 2018 10:31 UTC
  • Iran yaitaka dunia iheshimu uamuzi wa ICJ dhidi ya Marekani

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amezitaka nchi zote huru duniani kufungamana na uamuzi wa hivi karibuni wa Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ), kwa kutouinga mkono Marekani kuiwekea vikwazo Tehran.

Akilihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jana Alkhamisi, Gholamali Khoshroo amesema kuinga mkono Marekani katika kuiwekea vikwazo Iran ni ukiukaji wa agizo la mahakama na kitendo hicho hakitakuwa na matokeo mengine ghairi ya kuchochea zaidi mgogoro uliopo.

Ameongeza kuwa, vikwazo vya aina yoyote vinakiuka msingi wa diplomasia na mazungumzo na pia ni upuuzaji wa wazi wa mfumo wa sheria na ukiukaji wa haki za binadamu. Nchi nne za kundi la 5+1 zimetangaza kuwa zitaendelea kufungamana na JCPOA.

Nchi nyingi zimetangaza kuendelea kufungamana na JCPOA licha ya US kujiondoa na kutangaza vikwazo vipya dhidi ya Iran

Jumatano iliyopita, Federica Mogherini Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya alitoa taarifa akisisitiza umuhimu wa kulindwa makubaliano hayo ya nyuklia ya JCPOA ambyo ni matunda ya pamoja ya Umoja wa Mataifa na nchi za Ulaya. 

Mahakama hiyo ya ICJ yenye makao yake The Hague, Uholanzi Oktoba 3 ilitangaza hukumu yake kuhusu kesi iliyofunguliwa na Iran mwezi Julai mwaka huu dhidi ya Marekani, ambapo Tehran iliitaka mahakama hiyo iilazimishe Marekani isimamishe vikwazo vyake vya upande mmoja dhidi ya Iran baada ya Washington kujitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA mwezi Mei mwaka huu.

Mahakama hiyo iliiamuru Washington kusimamisha vikwazo vyake vya upande mmoja haraka iwezekanavyo dhidi ya Iran. Hata hivyo Washington ilisema uamuzi huo wa majaji wa ICJ hauna itibari na wala haitaufuata.