Rouhani: Nchi za Ulaya zikabiliane na Marekani kwa kushirikiana na Iran
(last modified Fri, 02 Nov 2018 06:08:12 GMT )
Nov 02, 2018 06:08 UTC
  • Rouhani: Nchi za Ulaya zikabiliane na Marekani kwa kushirikiana na Iran

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa sera za Marekani zimehatarisha uthabiti katika uga wa kimataifa na hivyo ametoa wito kwa nchi za Ulaya kushirikiana na Iran katika kukabiliana na maamuzi ya upande moja ya watawala wa Washington.

Rais  Rouhani amebainisha hayo Alhamisi katika makala aliyoiandika katika gazeti la Financial Times na kuongeza kuwa ushirikiano baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Ulaya utadhamini maslahi ya muda mrefu ya pande mbili na kuhakikisha kunapatikiana usalama na uthabiti kimataifa.

Katika makala yake hiyo, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitza kuwa sera za rais Donald Trump wa Marekani kuhusu masuala ya kibiashara, mikataba ya kimataifa na hata sera zake na waitifaki wa Marekani zimeibua changamoto mpya katika mfumo wa dunia. Rais Rouhani amesema sera za Marekani za maamuzi ya upande moja, ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya Waislamu, udhoofishaji mikataba ya kimataifa ukiwemo mkataba wa kulinda mazingira ni sera ambazo zinakinzana na muelekeo wa maamuzi yanayojumuisha pande kadhaa duniani. Aidha amesema sera hizo za Trump zinakinzana na mitazamo ya kisiasa na kijamii ya Ulaya.

Rais Rouhani ameendelea kusema kuwa hatua ya Marekani kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kama JCPOA ni sababu nyingine ambayo imepelekea kuvurugika uhusiano wa Ulaya na Marekani. Aidha amekumbusha kuwa Marekani imejiondoa katika mapatano hayo ya JCPOA ambayo yaliidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitia azimio 2231 na baada ya kujiondoa ikaiwekea Iran vikwazo vya upande moja. Rais Rouhani amesema Marekani sasa inatoa vitisho kwa nchi ambazo zinataka kutekeleza azimio hilo nambari 2231 la Umoja wa Mataifa na hatua kama hiyo ni dharau kwa sheria za kimataifa.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema sasa kuna udharura kwa nchi za Ulaya pamoja na Russia na China, kuwasilisha njia za kukabiliana na vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Iran ambayo vimepangwa kuanza Novemba 4.

 

Tags