Novemba 4; kukaribia siku ya mtihani mgumu kwa Umoja wa Ulaya
Siku tatu kabla ya kuanza awamu ya pili ya vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran, Rais Hassan Rouhani alizitaka nchi za Ulaya kusimama imara kukabiliana na mielekeo ya Washington ya kujichukulia hatua za upande mmoja.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu alitoa changamoto na wito huo katika andiko lake lililochapishwa na gazeti la Financial Times la Uingereza na kueleza kwamba: Kabla ya kuanza kutekelezwa vikwazo vipya vya upande mmoja na vya nje ya mipaka vya Marekani mnamo tarehe 4 Novemba, ni jambo la dharura kwa pande za Ulaya pamoja na Russia na China kutangaza na kuanza kutekeleza kifurushi rasmi cha hatua zao ambazo inapasa zichukuliwe ili kufidia athari za vikwazo vya Washington. Rais Rouhani alizionya pande zilizosalia katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kwa kusema: "Maafikiano haya ya kihistoria yataendelea kudumu ikiwa tu taifa la Iran litanufaika na matunda ya JCPOA."
Baada ya Marekani kujitoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji, JCPOA mnamo tarehe 8 Mei mwaka huu wa 2018, Iran ilitoa fursa kwa pande za Ulaya pamoja na China na Russia kufikiria utaratibu wa kuyaendeleza makubaliano hayo bila ya Marekani. Kufuatia hatua hiyo, yamefanyika mazungumzo ya mara kwa mara kati ya Iran na Ulaya, na hatimaye nchi za Ulaya zikaahidi kuwa, kabla ya kutekelezwa awamu mpya ya vikwazo vya Marekani, zitakuwa zimeshaanza kutekeleza utaratibu maalumu wa kifedha utakaowezesha kuendelezwa mabadilishano ya kibiashara na shughuli za kibenki baina yao na Iran.
Utaratibu maalumu wa mabadilishano ya kifedha uliopendekezwa na Umoja wa Ulaya unajulikana kama mfumo wa SPV, ambao lengo lake ni kuendeleza biashara na serikali ya Iran hata baada ya kuwepo vikwazo vya Marekani. Kinyume na mfumo wa mawasiliano ya kifedha wa SWIFT, ambao unaweza kufuatiliwa kimataifa, mfumo wa SPV utazihusisha nchi za Ulaya pekee, na wala Marekani haitaweza kufuatilia miamala inayofanywa kupitia mfumo huo. Sarafu ya dola ya Marekani haina nafasi katika mfumo wa Umoja wa Ulaya, na malipo yote ya fedha yanafanyika kwa kutumia sarafu ya yuro.
Hatua hiyo ya Umoja wa Ulaya inaakisi upinzani wa nchi za umoja huo kwa misimamo ya kujichukulia hatua za upande mmoja na kutokuwa tayari kuunga mkono vikwazo haramu vya Marekani, ikiwa ni ishara ya matunda ya diplomasia chanya na athirifu ya Iran ambayo imeifanya Washington itengwe kisiasa baada ya kujitoa kwenye makubaliano ya JCPOA. Kutekelezwa kivitendo mpango wa Umoja wa Ulaya wa SPV, sambamba na kuendelezwa biashara kati ya Iran na Russia, Uturuki na China kwa kutumia sarafu zao za taifa itakuwa ithibati ya kushindwa vikwazo vya Marekani na ushahidi kwamba sera hizo zilizochakaa na kupitwa na wakati haziwezi tena kuwa silaha ya kutumia ili kuyakomoa mataifa mengine. Kuhusiana na nukta hiyo, toleo la Jumatano iliyopita la gazeti la New York Times liliashiria ahadi iliyotolewa na Uingereza, Ufaransa na Ujerumani ya kuendeleza biashara na Iran na kuandika kuwa: "Hatua za Marekani za kukabiliana na Iran zimekabiliwa na vizuizi vikubwa."
Lakini mbali na hayo, ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya Russia, China na Iran na kuendelea India, Korea Kusini na China kununua mafuta ya Iran kumezidi kuzilemaza sera za vikwazo za Marekani. Sambamba na kukaribia tarehe 4 Novemba, Anatoly Aksakov, mkuu wa kamati ya masuala ya fedha ya bunge la Russia, Duma alitangaza siku ya Alkhamisi kwamba, Moscow na Tehran zinafanya mazungumzo kwa ajili ya kujiunga Iran na mfumo wa mabadilishano ya fedha wa ndani ya Russia uitwao SPFS.
Hatua zinazochukuliwa hivi sasa na nchi za Ulaya na za nje ya bara hilo zimevifanya vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran vikabiliwe na vizuizi vikubwa. Na hiyo ni nukta iliyobainishwa kwa uwazi katika kauli iliyotolewa hivi karibuni na mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani, John Bolton kuhusiana na kushindwa nchi hiyo kuiwekea vikwazo kamili vya mafuta Iran kwa kuifanya ishindwe kuuza mafuta yake kikamilifu. Jambo hilo limezusha tofauti na hitilafu kati ya viongozi wa Marekani kiasi cha kuwafanya baadhi yao waunge mkono kuendelea kuiruhusu Iran itumie mfumo wa mawasiliano wa kifedha, ujulikanao kama Jamii ya Mawasiliano ya Kifedha Baina ya Mabenki kwa ajili ya Ulimwengu Mzima, kwa kimombo The Society for Worldwide Interbank Financial Telecommunication (SWIFT).
Tathmini ya matukio kuhusiana na vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran inabainisha nukta muhimu na ya msingi ya kuwathibitishia walimwengu kwa mara nyengine tena kwamba, Iran haiko tayari kusalimu amri wala kulegeza msimamo katika hali yoyote ile. Ifahamike pia kwamba, hata kama pande zilizosalia katika makubaliano ya JCPOA nazo pia zitahalifu ahadi na makubaliano, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeshafikiria hatua za kuchukua kukabiliana na vikwazo vipya vya Marekani; kwa sababu manufaa na maslahi yake hayafungamani na makubaliano hayo ya nyuklia pekee.../