Ujerumani: Uhusiano wa kibiashara na Iran unapaswa kuendelea kuwepo
Msemaji wa serikali ya Ujerumani amesema kuwa, uhusiano wa kibiashara kati ya nchi hiyo ya bara Ulaya na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unapaswa kuendelea kuwepo.
Steffen Seibert amesema kuwa, ili kulinda na kuhifadhi uhusiano wa kibiashara na Iran, nchi yake inachunguza njia na mikakati ya lazima ili kuyalinda mashirika ya kibiashara na vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Iran.
Msemaji wa serikali ya Ujerumani amebainisha kwamba, kuna haja ya kuweko mikakati mbalimbali kwa ajili ya kulinda uhusiano wa kibiashara na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Matamashi hayo ya msemaji wa serikali ya Ujerumani yamekuja siku moja tu baada ya serikali ya Marekani jana tarehe 5 Novemba kuanza kutekeleza awamu nyingine ya vikwazo vyake vya kidhulma dhidi ya Iran ambavyo vinajumuisha sekta ya benki, mabadilishano ya kifedha na uuzaji wa mafuta ya Iran.
Nchi mbalimbali zinazounda Umoja wa Ulaya hususan washirika wa makubaliano ya nyuklia yaani Uingereza, Ujerumani na Ufaransa zimekuwa zikifanya kila ziwezalo kuhakikisha kwamba, zinapata njia za kukabiliana na vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Iran.
Tayari nchi hizo zikishirikiana na Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya zimetangaza kuwa, zimepiga hatua kubwa katika juhudi zao za kuanzisha mfumo maalumu wa kudumisha uhusiano wao wa kibiashara na kibenki na Iran bila ya kuathiriwa na vikwazo hivyo vya serikali ya Washington dhidi ya Tehran.