Nov 08, 2018 14:42 UTC
  • Louis Farrakhan, kiongozi wa harakati ya Nation of Islam ya Marekani amuonya Trump

Louis Farrakhan, kiongozi wa harakati ya Kiislamu ya Nation of Islam ya nchini Marekani amemtahadharisha vikali rais wa nchi hiyo Donald Trump kwamba asithubutu kuanzisha vita katika eneo la Mashariki ya Kati kwa kushinikizwa na utawala haramu wa Israel, akisisitiza kuwa matokeo ya vita hivyo yatakuwa mabaya mno.

Farrakhan ambaye yuko safirini hapa Iran amewaambia waandishi wa habari mjini Tehran leo Alkhamisi kuwa, "Namuomba rais (Trump) na serikali inayomuunga mkono kuwa waangalifu sana. Vita dhidi ya eneo la Mashariki ya Kati vitazilazimisha Russia na China kuingilia kati, na kama mnavyojua, vita hivyo vitaiangamiza Marekani."

Amesema, iwapo Trump atachochea vita katika eneo hilo, atasababisha kutokomezwa Marekani, dola kubwa zaidi duniani katika muda wa miaka mingi iliyopita.  

Loius Farrakhan akiwa mjini Tehran na maafisa wa ngazi za juu wa Iran

Kiongozi wa harakati hiyo ya Kiislamu ya nchini Marekani kadhalika ameukosoa vikali utawala wa Trump kwa kuanzisha duru mpya ya vikwazo dhidi ya Iran baada ya kuiondoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kubainisha kuwa, sera hasi za Trump ndizo zilizoeifanya dunia ikose imani naye na sasa anafanya Marekani izidi kutengwa kimataifa.

Loius Farrakhan siku chache zilizopita aliwahutubia wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tehran kwa mnasaba wa kumbukumbu ya miaka 39 ya Siku ya Kutekwa Pango la Ujasusi (Ubalozi wa Marekani) hapa mjini Tehran, na akawaongoza wanachuo hao kutoa kaulimbiu ya "Mauti kwa Marekani, mauti kwa Israel".

Louis Farrakhan alipata umashuhuri na kuwa shakhsia wa kimataifa kwa kuandaa kwa manikio makubwa Maandamano ya Watu Milioni Moja mjini Washington mwaka 1995, na amekuwa akitazamwa kama nembo ya Wamarekani wenye asili ya Afrika na kigezo cha uhamasishaji.

 

Tags