Hizbullah: Quds tukufu haiwezi kugawanyika
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i49745-hizbullah_quds_tukufu_haiwezi_kugawanyika
Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesema ni muhali na jambo lisiloyumkinika kuugawanya mara mbili mji mtukufu wa Quds (Jerusalem).
(last modified 2026-02-18T07:37:01+00:00 )
Nov 25, 2018 08:07 UTC
  • Hizbullah: Quds tukufu haiwezi kugawanyika

Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesema ni muhali na jambo lisiloyumkinika kuugawanya mara mbili mji mtukufu wa Quds (Jerusalem).

Sheikh Naim Qassim aliyasema hayo jana akihutubia Kongamano la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu hapa mjini Tehran na kusisitiza kuwa, ni jambo lisolowezekana kugawanya mipaka ya ndani ya taifa lolote lile, na kwa msingi huo Quds haiwezi kugawanishwa kuwe na ya mashariki na ya magharibi.

Huku akiitaja Marekani kuwa kilele cha jinai, ubeberu na dhulma duniani, Sheikh Qassim amesema utawala wa kifalme wa Aal-Saud na utawala wa Kizayuni wa Israel zinashirikiana na Washington kuuhujumu mji mtukufu wa Quds na Wapalestina kwa ujumla, na kwamba muqawama utashinda njama hizo za maadui.

Ameutaja utawala haramu wa Israel kuwa ni kitovu cha maovu na mzizi wa chuki, na kwamba lengo lake la kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina ni kurudisha nyuma gurudumu la maendeleo na ustawi katika eneo la Mashariki ya Kati.

Kongamano la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu

Mkutano wa 32 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu ulianza hapa mjini Tehran jana Jumamosi kwa kuwaleta pamoja washiriki zaidi ya 500 kutoka nchi 100 tofauti duniani, chini ya kaulimbiu ya "Quds, Mhimili wa Umoja katika Ummah."

Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon ameongeza kuwa, umoja, mshikamano na muqawama ndiyo mambo pekee yanayoweza kuwa chachu ya kuwashinda maadui wa ulimwengu wa Kiislamu.