Nov 25, 2018 16:13 UTC
  • Mkutano wa Umoja wa Kiislamu, Iran iko mstari wa mbele katika kambi ya kupigania uhuru

Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu unaendelea hapa mjini Tehran kwa kaulimbiu ya "Quds, Nguzo ya Umoja wa Umma". Mkutano huo wa siku tatu unahudhuriwa na shakhsia 300 wa kisiasa na kidini kutoka nchi mbalimbali duniani na unajadili njia za kutatua matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu.

Mkutano wa sasa wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu ambao hufanyika kila mwaka hapa nchini Iran katika siku za kuadhimisha Maulidi na kuzaliwa kwa Mtume wetu Muhammad (saw) una umuhimu mkubwa sana ukilinganishwa na mikutano 31 iliyopita. Mkutano huu ambao unahudhuriwa na wanafikra na wasomi wakubwa wa Umma wa Kiislamu ni ishara ya taathira ya sera za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran za kutaka kujenga na kuimarisha umoja baina ya Waislamu wote wa madhehebu tofauti na kutafuta njia za kukabiliana na changamoto zinazowakabili Waislamu kwa kutumia udugu wa Kiislamu. Mkutano wa mwaka huu pia unapata umuhimu maradufu kwa kutilia maanani njama inayotekelezwa na Marekani, Saudi Arabia, utawala haramu wa Israel na washirika wao iliyopewa jina la "Muamala wa Karne" ambayo inalenga kutokomeza kikamilifu malengo na Palestina, na vilevile juhudi zinazofanywa na serikali ya Washington za kujenga muungano wa kukabiliana na Iran. Kwa msingi huo miongoni mwa ajenda kuu za Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu wa Tehran ni kujadili njia za kuimarisha mapambano ya watu wa Palestina katika kalibu ya maandamano ya Haki ya Kurejea yanayofanyika kila siku ya Ijumaa huko katika Ukanda wa Gaza.

Maandamano ya watu wa Gaza dhidi ya Israel

Katika uwanja huo Naibu Mkuu wa Jumuiya ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu, Hussein Sheikhul Islam anasema: "Miongoni mwa masuala muhimu zaidi yanayojadiliwa katika Mkutano wa Kimataifa 32 wa Umoja wa Kiislamu ni suala la kurejea wakimbizi wa Palestina katika ardhi yao iliyoghusubiwa, sisitizo la kutetea haki zao za kisiasa na kisheria, njia za kukabiliana na njama mbalimbali zinazolenga kutokomeza kadhia ya Wapalestina, hali halisi ya eneo la Ukanda wa Gaza na jinsi ya kuwasaidia wakazi wa eneo hilo katika maandamano yao ya kila wiki ya Haki ya Kurejea.."

Vilevile kadhia ya Quds imepewa mazingatio makubwa katika mkutano wa sasa wa Umoja wa Kiislamu mjini Tehran hususan kwa kutilia maanani njama zinazofanywa na Marekani, Israel na vibaraka wao wa Kiarabu za kutaka kuwasahaulisha Waislamu eneo hilo takatifu. Fauzi al Alawi ambaye ni mhadhiri wa falsafa katika Chuo Kikuu cha Ez-Zitouna nchini Tunisia ambaye anashiriki mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu mjini Tehran anasema: "Miongoni mwa mambo yanayozidisha udharura wa kuwepo umoja baina ya Waislamu ni kadhia ya Palestina na Quds tukufu hususan wakati huu ambapo nchi za kikoloni zinataka suala hilo lipuuzwe, jambo ambalo linazusha mifarakano baina ya Waislamu."

Sehemu ya hadhirina katika Mkutano wa 32 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu mjini Tehran.

Suala jingine linalozidisha umuhimu wa Mkutano wa 32 wa Kimataiifa wa Umoja wa Kiislamu mjini Tehran ni mahudhurio ya wasomi, wanafikra na maulama wa Kiislamu zaidi ya 300 kutoka nchi mbalimbali duniani na kufanyika mkutano huu katika kipindi cha mashinikizo makubwa ya vita vya kinafsi na kiuchumi vya serikali ya Marekani dhidi ya Iran. Rais Donald Trump wa Marekani na tawala za Saudi Arabia na Israel zimefanya jitihada kubwa za kuhakikisha Iran inatengwa kimataifa. Hata hivyo mahudhurio makubwa ya wasomi, wanafikra, wanasiasa na viongozi wa kidini katika mkutano wa Tehran ni kielelezo cha kushindwa njama hizo khabithi za muungano wa Marekani.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu Ayatullah Muhsin Araki anasema: Marekani ikishirikiana na nchi na tawala nyingine kadhaa kama Saudi Arabia na utawala haramu wa Israel zimeanzisha vita vya kipropaganda dhidi ya Iran lakini kambi ya muqawama na mapambano inaendelea kusimama imara kukabiliana na njama hizo. 

Alaa kulli hal, mkutano wa sasa wa kimataifa wa Umoja wa Kiislamu mjini Tehran unatazamiwa kuchukua maamuzi muhimu kuhusu kadhia ya Palestina, Quds na njia za kuimarisha umoja na mshikamano baina ya Waislamu. 

Tags