May 22, 2024 14:56 UTC
  • Viongozi wa nchi 68 watoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa Sayyid Raisi na ya wenzake

Viongozi na maafisa wakuu wa nchi 68 duniani leo wamefika kwenye ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Tehran kutoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa Rais Sayyid Ebrahim Raisi na ya wenzake waliokufa shahidi pamoja naye katika ajali ya helikopta iliyotokea siku ya Jumapili.

Kwa mujibu wa IRNA, maafisa 68, wakiwemo viongozi wakuu wa nchi, maafisa wandamizi na wawakilishi wa mashirika ya kikanda na kimataifa leo walihudhuria hafla iliyoandaliwa na Kaimu Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwenye ukumbi wa mikutano wa Tehran ya kutoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa Sayyid Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ya wenzake waliokufa shahidi pamoja naye.

Amir wa Qatar, kiongozi wa taifa wa Turkmenistan, marais wa Tunisia, Syria na Tajikistan, mawaziri wakuu wa Pakistan, Iraq, Armenia, Jamhuri ya Azerbajan na Syria, Maspika wa mabunge ya Russia, Lebanon, Algeria, Kazakhstan, Mali, Ethiopia, na Mkuu wa Mabaraza la Juu la Uzbekistan, Mamakamu wa Rais wa Uturuki na India na Manaibu Mawaziri Wakuu wa Kyrgyzstan, Armenia, China, Afghanistan na Serbia ni miongoni mwa maafisa wakuu waliofika kwenye ukumbi wa mikutano wa Tehran kutoa mkono wa pole kwa Kaimu Rais na kutoa heshima zao za mwisho kwa Shahidi Sayyid Ebrahim Raisi na Mashahidi wenzake.

Viongozi wa nchi mbalimbali wakitoa heshima zao za mwisho kwa miili ya Mashahidi

Mawaziri wa mambo ya nje wa Lebanon, Misri, Tunisia, Saudi Arabia, Kuwait, Uzbekistan, Tajikistan, Belarus, Armenia, Azerbaijan, Sri Lanka, Afghanistan, Pakistan, Venezuela na Uturuki nao pia ni miongoni mwa maafisa wengine wa kigeni waliohudhuria hafla hiyo, ambapo mbali na kutoa mkono wa pole kwa Kaimu Rais walitoa heshima zao za mwisho kwa Shahidi Sayyid Ebrahim Raisi na Mashahidi wenzake.

Helikopta iliyokuwa imembeba Sayyid Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Jumapili jioni Mei 19, 2024 ilipata ajali ilipokuwa ikirejea kutoka kwenye hafla ya ufunguzi wa bwawa la Qiz Qalasi kwenye mpaka wa pamoja wa Iran na Jamhuri ya Azerbaijan.

Wakati helikopta hiyo ilipokuwa inaelekea mji wa Tabriz, ilianguka katika eneo la Varzghan mkoani Azarbaijan Mashariki, kaskazini-magharibi mwa Iran. Ndani yake walikuwemo pia Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje, Imam wa Ijumaa wa Tabriz, Gavana wa Azarbaijan Mashariki na watu wengine; na wote pamoja wakaifika hadhi tukufu ya kufa shahidi.../

 

Tags