Serikali ya Kabul yakaribisha juhudi za Iran za kurejesha amani Afghanistan
Serikali ya umoja wa kitaifa ya Afghanistan imekaribisha juhudi zinazofanywa na Iran za kurejesha amani nchini humo.
Fereidoon Khuzun msemaji wa Mkuu wa Baraza la Utekelezaji la Serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini Afghanistan amekaribisha jitihada zinazofanywa na Iran katika mchakato wa kurejesha amani nchini humo na kueleza kuwa, Tehran inafanya juhudi za kufanikisha mazungumzo kati ya makundi ya Kiafghani. Ameongeza kuwa, Iran imetoa ufafanuzi kwa serikali ya Afghanistan kuhusu jitihada hizo za kurejesha amani nchini humo. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hivi karibuni alithibitisha kwamba, ujumbe wa kundi la Taliban umefanya safari Tehran na kwamba ulikutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Iran chini ya uwenyekiti wa Sayyid Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa.
Ushirikiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na serikali ya Afghanistan katika kusaidia juhudi za kurejesha amani na utulivu nchini humo si jambo jipya. Hii ni kwa sababu siasa kuu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuiunga mkono serikali, kujitawala na mamlaka ya kitaifa ya Afghanistan. Vahid Mojde mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Afghanistan amesema: Bila shaka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina mchango mkubwa katika kuyapatia ufumbuzi matatizo ya Afghanistan. Kwa msingi huo kuna udharura wa kutumiwa uwezo wake katika mchakato wa kurejesha amani nchini Afghanistan.
Kwa msingi huo Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia inafanya jitihada kubwa za kufanikisha mchakato huo wa mazungumzo baina ya serikali ya Afghanistan na kundi la Taliban. Hakuna shaka kwamba, kurejesha amani na usalama huko Afghanistan kuna maslahi kwa nchi zote za eneo hili, na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia siku zote inasisitiza suala la kufanyika mazungumzo kati ya makundi yote ya Kiafghani ili kurejesha amani nchini humo. Tajiriba ya miaka kadhaa ya kuwepo hali ya mgogoro na machafuko huko Afghanistan inaonyesha kuwa, uingiliaji kati wa nchi ajinabi hususan zile za mbali katika masuala ya ndani ya Afghanistan si tu kuwa umezidisha mgogoro na hali ya mchafukoge nchini humo bali pia umeifanya hali ya mambo ya nchi hiyo kuwa mbaya zaidi.
Kwa sababu hiyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inazitolea wito pande husika katika mgogoro wa Afghanistan kuketi kwenye meza ya mazungumzo na kuunga mkono mchakato wa kurejesha amani nchini humo na inaamini kuwa, kundi la Taliban pia linapasa kusaidia juhudi za kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo kwa njia za kisiasa kwa kutambua vyema hali ya mambo na kubadili misimamo yake. Hii ni kwa sababu zama za vita na umwagaji damu nchini humo zimepita na wananchi wa Afghanistan wanataraji kuwa, makundi yote nchini humo yatashirikiana katika kutatua mgogoro unaoisumbua nchi yao kwa miaka mingi sasa.
Abdulatif Nazari mhadhiri wa chuo kikuu katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul anazungumzia nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kufanikisha mchakato wa amani nchini Afghanistan akisema kwamba: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa nchi yenye nguvu na yenye taathira katika eneo hili imekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha hali ya usalama na utulivu wa kisiasa nchini Afghanistan. Safari ya karibuni ya maafisa wa Iran mjini Kabul kwa lengo la kupanua uhusiano na ushirikiano wa kisiasa, kitamaduni na kiusalama kati ya Afghanistan na Jamhuri ya Kiislamu ilikuwa na manufaa makubwa.
Alaa kulli hal, nukta ya kuzingatia hapa ni kuwa, wananchi wa Afghanistan wanataraji kuliona kundi la Taliban lenyewe likijitambua kuwa ni kundi la kitaifa. Hii ina maana kwamba, kundi hilo linapaswa kusaidia jitihada za maendeleo na ustawi wa Afghanistan kwa kushirikiana na serikali na taasisi mbalimbali za kiraia za nchi hiyo. Kwani Waafghani pia wamechoshwa na vita vya miaka mingi sasa na wanahitaji kukilea kizazi kijacho cha nchi hiyo katika kivuli amani; kwa njia hiyo katika mustakbali Afghanistan iweze kupata nguvu na uwezo wa kulinda uhuru na mamlaka yake ya kitaifa.