Feb 10, 2019 14:12 UTC
  • Zarif: Mkutano wa Marekani dhidi ya Iran umefeli hata kabla haujaanza

Waziri wa Mambo ye Nje wa Iran amesema mkutano wa Marekani unaotazamiwa kufanyika nchini Poland katika siku chache zijazo na ulio dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umefeli hata kabla haujaanza.

Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo katika mahojiano na shirika la habari la ICANA na kuongeza kuwa, hatua ya Marekani kubadili anuani ya mkutano huo siku chache kabla ya kufanyika ni ishara tosha kuwa kikao hicho kimefeli hata kabla ya kufunguliwa.

Amesema, "Marekani inataka kufidia mazingira yaliyojengwa dhidi yake, na inavyoonekana, mkutano huo hautafanyika kama walivyotaka Wamarekani wenyewe."

Dakta Zarif amesema jambo la pili linaloashiria kushindwa kufikia malengo yaliyotarajiwa katika kikao hicho, ni kitendo cha Marekani kusema kuwa mkutano huo utahudhuriwa na Naibu Rais wa nchi na wala sio rais, kama ilivyokuwa imeripotiwa hapo awali.

Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ni miongoni wa watu watakaoshiriki kikao cha Warsaw

Palestina na Russia ni miongoni mwa nchi zilizotangaza kuwa hazitahudhuria mkutano wa hapo tarehe 13 na 14 mwezi huu wa Februari huko Warsaw mji mkuu wa Poland, uliopewa anwani ya "Mkutano wa Amani na Usalama katika Mashariki ya Kati".

Baada ya Mkuu wa Sera za Kigeni za Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini na nchi kadhaa za dunia kusema kuwa hazitashiriki mkutano huo, serikali ya Washington ilibadili kaulimbiu ya kikao hicho cha Warsaw kutoka 'Mkutano dhidi ya Iran' na kuuita mkutano kuhusu eneo la Mashariki ya Kati.

Tags