Bahman 22 katika miaka 40 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu
(last modified Mon, 11 Feb 2019 17:21:42 GMT )
Feb 11, 2019 17:21 UTC
  • Bahman 22 katika miaka 40 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Leo Jumatatu tarehe 11 Februari 2019 ambayo imesadifiana na tarehe 22 Bahman 1397 kwa mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsia, ni siku ambayo zimefikia kileleni sherehe za miaka 40 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Kujitokeza kwa wingi na kwa mshikamano mkubwa wananchi wa Iran katika maandamano ya Bahman 22 katika miaka yote hii, kumekuwa ni nembo ya istiqama, umoja na sherehe ya ushindi wa taifa la Iran dhidi ya mfumo wa kibeberu duniani. 

Mwaka huu pia, kujitokeza huko wananchi katika maandamano hayo kumeonesha kwa uwazi kabisa na kwa mara nyingine tena; umoja na mshikamano wa taifa la Iran ambalo limetangaza tena utiifu wake kwa malengo matakatifu ya Mapinduzi ya Kiislamu kwa shauku na matumaini ya dhati ya mustakbali mwema. Maadui wa taifa la Iran wanautambua vyema uhakika huo na ndio maana wanafanya njama za kila namna kuwakatisha tamaa na kuwachosha wananchi, taifa la Iran na mapinduzi yao matukufu ya Kiislamu.

Rais Hassan Rouhani akiwa katikati ya maandamano ya Bahman 22 kuadhimisha miaka 40 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu

 

Ukweli wa mambo ni kuwa, Marekani imejikita kwenye masuala matatu makuu katika kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu na kwenye vita vyake laini dhidi ya taifa la Iran.

Mosi ni kujaribu kuufutia itibari mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kujaribu kuonesha umejaa ufisadi katika sehemu mbalimbali.

Pili ni kujaribu kuondoa imani ya wananchi kwa Jamhuri ya Kiislamu na kujaribu kuonesha kuwa mfumo huo wa utawala haufai.

Na tatu ni kujaribu kuzusha utengano baina ya wananchi na Jamhuri ya Kiislamu kwa kutumia vikwazo vya kulemaza uchumi wa Iran na kujaribu kuzusha malalamiko na uasi wa kijamii.

Hata hivyo taifa la Iran limeibuka na ushindi katika kipindi chote hiki cha miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu, licha ya kukumbwa na mitihani mikubwa na migumu kama vile vita na vikwazo vya kila upande vya kiuchumi. Katika miaka yote hiyo, hakuna kitu chochote kilichoweza kuteteresha imani na irada ya taifa la Iran ya kuendelea mbele na njia ya mapinduzi yake matukufu ya Kiislamu.

Watu wa makabila na kaumu tofauti hushirikiana kwa pamoja kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran

 

Kwa hakika ni sawa kabisa alivyosema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa: "Ni kweli kwamba katika baadhi ya sehemu mambo hayakutendeka ilivyotarajiwa na Mapinduzi (ya Kiislamu), lakini pembeni mwa hilo kuna mafanikio mengi makubwa zaidi tuliyopata; kustawi na kusonga mbele Mapinduzi (ya Kiislamu) ndio muujiza wa mapinduzi haya." 

Ukweli ni kwamba taifa la Iran lilifanya mapinduzi ili kuwa huru na kuwa na heshima. Uhuru na heshima ya taifa la Iran haimalizikii tu katika mahitaji ya kiuchumi na kimaisha. Mapinduzi huwa ni maandalizi ya kutokea harakati kubwa zaidi ambazo haziwezi kufanikiwa isipokuwa kwa kusimama imara mbele ya mambo mazito na kutosalimu amri mbele ya mashinikizo. Ni kwa kujipamba kwa subira na uvumilivu na wakati huo huo kuwa na tadibiri na kutegemea uwezo wake mkubwa wa ndani ndio maana taifa la Iran limeweza kumakinisha thabiti nafasi yake ya kuendelea na mapinduzi yake matukufu ya Kiislamu yenye utulivu na taathira kubwa ndani na nje ya nchi. Leo pia taifa la Iran limesimama imara vile vile kwa shauku, msukumo na hamasa kubwa zaidi kuliko huko nyuma katika kulinda malengo yake matukufu na huo ni uhakika ambao hauendani kabisa na mahesabu ya viongozi wa Marekani. 

Katika moja ya miongozo yake ya busara, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alizungumzia kuwepo matatizo ya kiuchumi humu nchini na kusema: Wamarekani wameghiriki katika njozi zao kwa kutegemea matatizo hayo, jambo ambalo linaonesha akili zao finyu na ukosefu wao wa tadibiri

Mvua ya theluji iliyonyesha leo katika maeneo tofauti ya Iran haikuwazuia kabisa wananchi kujitokeza katika maadhimisho ya Bahman 22 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu

 

Ni hivi karibuni tu ambapo rais wa Marekani aliwaambia baadhi ya viongozi wa Ulaya kuwa, kama watasubiri miezi miwili mitatu tu ijayo, basi wataona Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haipo tena. Njozi na ndoto hizo zinatukumbusha matamshi ya miaka 40 iliiyopita ya viongozi wa Marekani na vibaraka wao wa ndani ambao walipeana matumaini ya kupinduliwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi cha miezi sita tu, lakini sasa hivi mfumo huu wa Kiislamu umetimiza miaka 40 ukiwa imara zaidi kuliko wakati mwingine wowote.

Ujumbe wa maandamano ya leo ya Bahaman 22 ya wananchi wa Iran yaliyofana sana kuliko miaka yote ya huko nyuma; ni sisitizo jingine la kusimama imara mbele ya uadui wa madola ya kibeberu na kiistikbari na ni majibu kwa vitisho na maneno kama yale ya White House ya eti machaguo yote hata ya kijeshi yako mezani dhidi ya taifa la Iran.

Shauku na hamasa hii kubwa iliyooneshwa leo na wananchi wa Iran katika kipindi hiki cha kuanza muongo wa 5 wa Mapinduzi ya Kiislamu tunapaswa kuihesabu kuwa ni nukta nzuri mpya ya heshima na ushind kwa taifa la Iran.

Tags