Qassemi: Iran haiwaombi wengine ruhusa kuhusu masuala yake ya ndani na nje
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haikubali masharti na haiwaombi wengine ruhusa kuhusu masuala yake ya ndani ya nje.
Bahram Qassemi ameongeza kuwa ushawishi wa kieneo ilionao Iran ambao unazifanya Marekani na utawala wa Kizayuni kutekeleza njama mbalimbali ni ushawishi wa wananchi na wa dhati na ambao hauhusiani na hatua mahsusi ya serikali wala utawala ulioko madarakani. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameyasema hayo leo Jumatatu katika kikao cha kila wiki na waandishi habari wa ndani na nje hapa Tehran kuhusu baadhi ya taarifa zilizochapishwa kuhusiana na masharti ya Umoja wa Ulaya ya kupunguzwa ushawishi wa Iran katika eneo mkabala na kupanua ushirikiano wa pande mbili.
Qassemi amebainisha kuwa ushawishi wa kimaanawi na kieneo wa Iran si suala ambalo linaweza kupunguzwa au kuzidishwa kwa ombi la nchi moja au mbili na kwamba Iran itasogeza mbele siasa zake za kieneo na kimataifa kwa uhuru kamili ilionao.
Kuhusu safari ya karibuni ya Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia huko Pakistan na uhusiano wa nchi hiyo na Iran, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: Uhusiano wa Tehran na Islamabad ni wa siku nyingi na nchi mbili hizi jirani zinatilia maanani uhusiano mwema baina ya majirani.
Ameongeza kuwa hitilafu zilizojitokeza hivi karibuni katika uhusiano wa Iran na Pakistan baada ya kujiri shambulio la kigaidi huko Sistan Balochistan hazikuwa takwa la nchi hiyo na kwamba wakati huo huo Iran imeitaka Pakistan ishughulikie na kufuatilia kwa dhati suala la kudhamini usalama wa mipaka ya nchi mbili na kuwepo mawasiliano endelevu kati ya Iran na Pakistan katika uwanja huo.