Mar 15, 2019 15:47 UTC
  • Ayatullah Kashani: Taifa la Iran halitasalimu amri mbele ya mashinikizo ya maadui

Khatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa mjini Tehran amesema maadui wamekuwa wakitumia njama mbalimbali kama za kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni ili kutoa pigo kwa mfumo wa Kiislamu unaotawala hapa nchini Iran, lakini amesisitiza kuwa, katu taifa kubwa la Iran haliwezi kusalimu amri mbele ya mashinikizo ya maadui.

Ayatullah Muhammad Emami Kashani amesema hayo leo mbele ya hadhara kubwa ya waumini waliohudhuria ibada ya Swala ya Ijumaa mjini Tehran ambapo ameyaasa na kuyataka mataifa ya Kiislamu kuwa macho na njama za maadui dhidi yao.

Ayatullah Kashani ameashiria hotuba ya hivi karibu ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye alionya kuwa, Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel zinafanya kila ziwezalo ili kueneza kampeni zao za kiuhasa dhidi ya taifa la Iran, lakini umoja na mshikamano umetoa pigo kwa adui. 

Amefafanua kuwa, ulimwengu wa Kiislamu hii leo unakabiliwa na njama mbalimbali za baadhi ya madola ya Magharibi na ya Kiarabu yanayoyaunga mkono makundi ya kigaidi na kitakfiri ikiwemo Saudi Arabia na kusisitiza kwamba, mataifa ya Kiislamu hayapaswi kusalimu amri mbele ya njama hizo.

Ayatullah Kashani akiongoza Sala ya Ijumaa mjini Tehran

Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran amebainisha kuwa: "Dunia hii leo inatambua nafasi ya Iran katika kupambana na ugaidi. Dunia inajua kuwa Iran imeishinda Marekani na njama zake ghalati katika nchi za Syria na Iraq."

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Kashani amesisitiza umuhimu wa maafisa na viongozi wa serikali kufanya juhudi kwa ajili ya kutatua matatizo ya kiuchumi yanayowakabili wananchi.

Tags