Vikwazo vya dawa dhidi ya Iran; Mahakama ya ICJ yaitaka Marekani ijieleze
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i52525-vikwazo_vya_dawa_dhidi_ya_iran_mahakama_ya_icj_yaitaka_marekani_ijieleze
Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ) imesema, imeipeleka barua serikali ya Marekani kuitaka iondoe vikwazo ilivyoiwekea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Mar 31, 2019 03:09 UTC
  • Vikwazo vya dawa dhidi ya Iran; Mahakama ya ICJ yaitaka Marekani ijieleze

Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ) imesema, imeipeleka barua serikali ya Marekani kuitaka iondoe vikwazo ilivyoiwekea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Mohsen Mohebi, mwakilishi wa Iran katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu alitangaza jana kuwa: Siku ya Ijumaa, mahakama hiyo iliipelekea barua serikali ya Marekani na kuitaka hadi ifikapo tarehe 16 Mei mwaka huu, iwe imeshaeleza ni hatua gani imechukua kwa ajili ya kutekeleza amri ya mahakama hiyo ya kimataifa ya uadilifu, kuhusiana na kuondoa vikwazo vya dawa, chakula, vipuri vya ndege na huduma za anga dhidi ya Iran.

Tarehe 3 Oktoba 2018, Mahakama ya ICJ ilitangaza kuwa, inayo mamlaka kisheria ya kusikiliza lalamiko la Iran dhidi ya Marekani kwa sababu ya kukiuka mkataba wa urafiki na uhusiano wa kiuchumi na sheria za kibalozi wa mwaka 1955 uliofungwa na nchi hizo mbili; na ikaitaka Washington iondoe vikwazo vya ununuzi wa dawa, chakula, masuala ya binadamu na vya anga ilivyoiwekea Iran.

Jaji Abdulqawi Ahmed Yusuf wa Mahakama ya ICJ akisoma sehemu ya uamuzi uliotolewa mwezi Oktoba

Barua ya Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu kwa serikali ya Marekani imetupilia mbali madai ya nchi hiyo kwamba eti vikwazo ilivyoiwekea Iran havijumuishi dawa na chakula. Kujitoa kimasomaso na kuonyesha huruma za mamba kunakofanywa na serikali ya sasa ya Marekani kwa kuonyesha inawahami na kuwaunga mkono wananchi wa Iran kumedhihirika kuwa ni uongo baada ya Washington kukiuka kanuni za masuala ya kibinadamu; na hatua iliyochukua ya kuiwekea vikwazo Iran baada ya kujitoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, imewalenga moja kwa moja raia wa kawaida wa Iran.

Kuweka vikwazo dhidi ya ununuzi wa dawa na chakula na kuifungia nchi njia za angani, ardhini na baharini isiweze kujidhaminia mahitaji ya huduma za kibinadamu hakuendani na sheria yoyote ya kimataifa. Muelekeo unaofuatwa na serikali ya Marekani, unaonyesha uhasama na uadui ilionao kwa taifa la Iran, ambapo Washington imeamua kutumia kila njia ili kuweza kufikia malengo yake haramu na ya utumiaji mabavu.

Kitendo cha serikali ya Marekani kutumia msamiati wa 'kulidhikisha kwa njaa' taifa la Iran kimewadhihirishia walimwengu upeo wa juu kabisa wa uadui ilionao Washington kwa taifa imara la Iran; taifa ambalo kwa muda wote wa miaka 40 iliyopita halijakubali katu kusalimu amri mbele ya Marekani licha ya kuandamwa na misukosuko na tabu mbalimbali; na hivi sasa limeuanza muongo wa tano wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa fahari na heshima kubwa.

Kuwa bega kwa bega wananchi na mfumo wao wa Jamhuri ya Kiislamu kumeifanya Iran iwe nchi yenye nguvu, satua na ushawishi; na kuwawezesha wananchi hao na mfumo wao kuzivuka kwa pamoja awamu na vipindi vigumu ya Mapinduzi ya Kiislamu; na hii leo pia watakivuka kizingiti kirefu cha vikwazo kwa ungangari na mshikamano wao.

Kwa hakika uamuzi wa Marekani wa kutumia silaha ya vikwazo ni ishara ya kukataa tamaa Washington katika kukabiliana na taifa la Iran. Marekani haioni aibu hata chembe kutumia silaha ya haki za binadamu kwa ajili kufikia malengo yake; na kama itafika mahala ikagonga mwamba katika hilo, basi huamua kuyawekea hata vikwazo vya dawa na chakula mataifa yenye msimamo wa muqawama.

Katika hali kama hiyo, kuishtaki serikali ya Marekani ni haki ya kila nchi; na kutokana na nchi hiyo kujitoa kwenye makubaliano ya JCPOA na kurejesha vikwazo vya kidhalimu dhidi ya Iran, Jamhuri ya Kiislamu imewasilisha malalamiko yake dhidi ya Washington katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu. Na baada ya mahakama hiyo kuthibitisha kuwa Marekani imeiwekea Iran vikwazo hata vya ununuzi wa dawa na chakula imetoa hukumu ya kutaka vikwazo hivyo viondolewe.

Hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu imeeleza bayana kuwa, vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya wananchi wa Iran ni haramu kisheria. Katika hali kama hiyo kudharau serikali ya sasa ya Marekani uamuzi uliopitishwa kwa kauli moja na jopo la mahakimu wa ICJ kutaibebesha Washington masuulia kimataifa; na nchi yoyote ile itakayoshirikiana nayo katika kutekeleza vikwazo dhidi ya wananchi wa Iran itahesabika kuwa imeisaidia serikali halifu ya rais wa Marekani Donald Trump.

Kuhusiana na nukta hiyo, balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini The Hague, Alireza Jahangiri amesema: Mbali na Marekani, uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu una ulazima wa kutekelezwa na nchi nyingine zote; na Marekani pamoja na nchi zingine duniani, zina wajibu wa kujiepusha na kuliwekea mipaka na vizuizi taifa la Iran.../