Apr 12, 2019 15:15 UTC
  • Wairani waandamana kote nchini kuliunga mkono Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH)

Wananchi wa Iran katika kila kona ya nchi wamemiminika mabarabarani kushiriki maandamano ya kuonyesha uungaji mkono wao kwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH.

Maandamano hayo yamefanyika baada ya Sala ya Ijumaa katika takriban miji yote mikubwa ya nchi, ukiwemo mji mkuu Tehran. Baadhi ya waandamanaji walikuwa wamebeba mabango na maberamu yenye jumbe za kuliunga mkono na kulipongeza jeshi la IRGC.

Aidha waandamanaji hao wamesikika wakipiga nara za 'Mauti kwa Marekani' na 'Mauti kwa Israel'.

Wakati huohuo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameonya kuwa, Marekani na vibaraka wake katika eneo wawe tayari kubeba dhima kwa matokeo mabaya yatakayosababishwa na hatua hiyo ya kiuhasama ya Washington dhidi ya IRGC.

Wanawake wa Iran katika maandamano ya kuiunga mkono SEPAH

Mohammad Javad Zarif amebainisha hayo katika barua aliyomtumia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres na Baraza la Usalama la UN na kuongeza kuwa, kitendo hicho ni ukiukaji wa wazi wa Hati ya Umoja wa Mataifa na misingi ya sheria za kimataifa.

Amesema, "Hatua ya serikali ya Marekani ambayo haijawahi kushuhudiwa tena, ambayo ni kinyume cha sheria na hatari ya kuliweka tawi rasmi la Vikosi vya Iran katika orodha ya makundi ya kigaidi ni ya kichokozi na kiuhasama kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na ni tishio kubwa kwa usalama na amani ya kieneo na kmataifa."

 

 

Waandamanaji wakiwa na mabango mjini Qum

Siku ya Jumatatu, utawala wa Marekani ulitangaza kuliweka Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika orodha yake ya makundi ya kigaidi.

Kufuatia uhasama huo wa Marekani, Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limetangaza kuwa, wanajeshi wote wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi (CENTCOM) na vikosi vyote vinavyofungamana nao ni kundi la kigaidi.

Hata vijana wameshiriki maandanano ya leo

 

Tags