Kamati ya Nyuklia ya Iran: Tutajiondoa NPT, JCPOA iwapo tutaendelea kuwekewa vikwazo
Mwenyekiti wa Kamati ya Nyuklia ya Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema iwapo taifa hili litaendelea kukabiliwa na vikwazo, basi Tehran itajitoa katika Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezaji wa Silaha za Atomiki (NPT) sambamba na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Katika mahojiano na shirika la habari la Mehr, Mojtaba Zonnour amesema kuwa, katika hali ambayo Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu haujafikia uamuzi wa kuindoa nchi hii katika mikataba hiyo ya kimataifa, lakini kamati hiyo ya Bunge la Iran inatafakari kuhusu mpango huo, iwapo itaendelea kuandamwa na vikwazo vya kidhalimu.
Amefafanua kuwa, "tukiendelea kukabiliwa na vikwazo, hatutakuwa na sababu ya kuendelea kushirikiana na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA); na kujiondoa kwenye Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezaji wa Silaha za Atomiki (NPT) sambamba na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni miongoni mwa machaguo tuliyo nayo mezani."
IAEA imethibitisha mara 15 kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetekeleza ahadi zake kuhusiana na makubaliano ya JCPOA. Mnamo Mei 2018, Marekani ilichukua uamuzi wa upande mmoja wa kujiondoa katika mapatano ya kimataifa ya JCPOA, hatua ambayo imeendelea kukosolewa vikali kimataifa na kupelekea watawala wa Washington kuzidi kutengwa.
Huku akiashiria kuhusu azma ya Washington ya kutaka kukata kimilifu uuzaji wa mafuta ya Iran nje ya nchi, Mwenyekiti wa Kamati ya Nyuklia ya Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema ni jambo lisilowezekana kwa Marekani kufanya uuzaji wa mafuta ya Iran ufikie kiwango cha sifuri, kwani Jamhuri ya Kiislamu ina wateja wake, na inafahamu mbinu za kuendelea kuuza mafuta yake."
Mojtaba Zonnour amesisitiza kuwa, Iran ina uwezo na ujuzi wa kushughulikia mabadilishano yake ya kifedha licha ya vikwazo na mashinikizo ya Marekani.