NATO: Taarifa za Marekani kuihusu Iran si kinaifu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i53560-nato_taarifa_za_marekani_kuihusu_iran_si_kinaifu
Afisa mmoja wa kitengo cha upelelezi wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi NATO amekosoa taarifa zinazotolewa na Marekani kuhusu maandalizi ya Iran kwa ajili ya kushambulia maslahi ya Marekani katika eneo na kuongeza kuwa, taarifa hizo kuihusu Tehran si za kukinaisha na hata ni za kudhalilisha.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 18, 2019 07:47 UTC
  • NATO: Taarifa za Marekani kuihusu Iran si kinaifu

Afisa mmoja wa kitengo cha upelelezi wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi NATO amekosoa taarifa zinazotolewa na Marekani kuhusu maandalizi ya Iran kwa ajili ya kushambulia maslahi ya Marekani katika eneo na kuongeza kuwa, taarifa hizo kuihusu Tehran si za kukinaisha na hata ni za kudhalilisha.

Afisa huyo wa NATO amesema kuwa, juhudi za Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kwa ajili kutafuta uungaji mkono wa Ulaya kwa madhumuni ya kuikabili Iran, zimekabiliwa upinzani wa Ulaya. Ameongeza kwamba, maelezo ya Pompeo kuihusu Iran ni uvumi na yanatokana na vyanzo dhaifu visivyofaa kutegemewa.

Katika siku kadhaa zilizopita, Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alifanya safari nchini Iraq, Russia na Ubelgiji kwa ajili ya kutafuta uungaji mkono dhidi ya Iran, ingawa hata hivyo alirejea Washington akiwa mikono mitupu. 

Wakati huo huo Rais Donald Trump wa Marekani ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twetter akikosoa habari zisizo na ukweli wowote zinazoenezwa na vyombo vya habari vya nchi hiyo kuhusiana na mgogoro uliopo kati ya Marekani na Iran na kusema kuwa, habari hizo ni bandia.

Baadhi ya viongozi wa timu ya Trump

Trump aliyasema hayo Ijumaa ya jana na kusema kuwa, habari zinazoenezwa na vyombo vya habari vya nchi yake juu ya Iran ni bandia. ‘Hatua ya vyombo vya habari kutangaza taarifa zisizo sahihi kuhusu Iran, inaisababishia madhara Marekani.’ Amesema rais huyo wa Marekani. Kadhalika Trump amekosoa misimamo ya kugongana na ya hadaa ya viongozi wa White House kuhusiana na Iran na kusema: ‘Uenezaji huo wa habari kupitia hadaa, na unaotegemea vyanzo bandia, ni hatari sana.’

Itakumbukwa kuwa tarehe 14 ya mwezi huu Trump alikadhibisha madai ya gazeti moja la Kimarakeni juu ya mpango wa Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo (Pentagon) kwa ajili ya kutuma askari laki moja na elfu 20 kuelekea eneo la Asia Magharibi kwa ajili ya kukabiliana na Iran na kuitaja habari hiyo kuwa ni bandia.