Iran yasema vita havitaibuka katika eneo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i53582-iran_yasema_vita_havitaibuka_katika_eneo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mohammad Javad Zarif amesema hakuna vita vitakavyoibuka Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) pamoja na kuwepo hali ya taharuki baina ya Iran na Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 19, 2019 03:27 UTC
  • Iran yasema vita havitaibuka katika eneo

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mohammad Javad Zarif amesema hakuna vita vitakavyoibuka Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) pamoja na kuwepo hali ya taharuki baina ya Iran na Marekani.

Katika mahojiano na Shirika la Habari la IRNA Jumamosi, Zarif amebaini kuwa: "Kama alivyosema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, tuna yakini kuwa vita havitaibuka kwani sisi  hatutaki vita na pia hakuna mwenye dhana au fikra kuwa anaweza kukabiliana na Iran katika eneo."

Jumatano iliyopita, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyed Ali Khamenei alisema hakutatokea vita baina ya Marekani na Iran na akaongeza kuwa, Marekani inafahamu vyema kuwa vita kama hivyo havitakuwa kwa maslahi yake. Huku akiashiria njama za Marekani zilizo dhidi ya Tehran alisema kuwa, chaguo hasa la taifa la Iran katika kukabiliana na adui ni mapambano na muqawama kwenye nyuga zote, na katika mapamabano hayo Marekani italazimika kurudi nyuma.

Zarif ameongeza kuwa, Rais Donald Trump wa Marekani hataki vita lakini kuna watu wanaomzunguka ambao wanataka kumsukuma kuelekea katika vita.

Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema wapenda vita katika 'Timu B' inayoundwa na Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani John Bolton, Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia na Bin Zayed mrithi wa kiti cha ufalme wa Imarati (UAE) wanajaribu kuisukuma Marekani kuanzisha vita vya kijeshi dhidi ya Iran.

Wiki iliyopita, gazeti la New York Times liliripoti kuwa, Trump amewaamuru maafisa wa utawala wake kujiepusha na makabiliano ya kijeshi na Iran.

Msuguano baina ya Iran na Marekani ulianza mwezi Mei 2018 baada ya Rais Trump kuiondoa nchi yake katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji (JCPOA). Baada ya hapo Washington ilirejesha tena vikwazo dhidi ya Iran hatua ambayo inaendelea kulaaniwa kimataifa. Marekani sasa imeanzisha vita vya kisaikolojia dhidi ya Iran kwa kutumua meli zake za kivita katika eneo.