Kamanda wa IRGC: Iran haitaki vita, lakini pia haiogopi vita
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i53589-kamanda_wa_irgc_iran_haitaki_vita_lakini_pia_haiogopi_vita
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) Meja Jenerali Hussein Salami amesema kuwa Iran haitaki vita lakini pia wakati huo huo haiogopi vita.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
May 19, 2019 10:00 UTC
  • Kamanda wa IRGC: Iran haitaki vita, lakini pia haiogopi vita

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) Meja Jenerali Hussein Salami amesema kuwa Iran haitaki vita lakini pia wakati huo huo haiogopi vita.

Akizungumza mjini Tehran leo Jumapili, Meja Jenerali Salami amesema hivi sasa Iran inakabiliana na vitisho karibu na mipaka yake na hivyo IRGC imejiweka tayari kukabiliana na vitisho hivyo. Kamanda wa IRGC amesisitiza kuwa, Iran haitaki kuwa mwenye kuanzisha hujuma. Akifafanua zaidi Meja Jenerali  Salami amesema: "Hatufuatilii vita lakini pia hatuogopi vita ingawa maadui walio mbele yetu hawana irada ya kuanzisha vita na wanaogopa mapigano."

Kamanda wa IRGC amesisitiza kuwa hivi sasa sekta ya ulinzi ya Iran iko katika utayarifu wa hali ya juu.

Kwingineko katika hotuba yake, Brigedia Jenerali Salami amesema nguvu za Marekani zinaonekana kidahiri tu. Amesema kuwa leo tunashuhudia kupungua uwezo wa Marekani hatua kwa hatua na katika mustakabali wa karibu tutashuhudia kusambaratika nguzo ambazo zimekuwa zikiishikilia Marekani.

Wiki iliyopita, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyed Ali Khamenei alisema hakutatokea vita baina ya Marekani na Iran na akaongeza kuwa, Marekani inafahamu vyema kuwa vita kama hivyo havitakuwa kwa maslahi yake. Huku akiashiria njama za Marekani zilizo dhidi ya Tehran alisema kuwa, chaguo hasa la taifa la Iran katika kukabiliana na adui ni mapambano na muqawama kwenye nyuga zote, na katika mapambano hayo Marekani italazimika kurudi nyuma.

Makombora ya Iran

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif katika mahojiano na Shirika la Habari la IRNA Jumamosi, amebaini kuwa: "Kama alivyosema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, tuna yakini kuwa vita havitaibuka kwani sisi  hatutaki vita na pia hakuna mwenye dhana au fikra kuwa anaweza kukabiliana na Iran katika eneo."

Msuguano baina ya Iran na Marekani ulianza mwezi Mei 2018 baada ya Rais Trump kuiondoa nchi yake katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA). Baada ya hapo Washington ilirejesha tena vikwazo dhidi ya Iran hatua ambayo inaendelea kulaaniwa kimataifa. Marekani sasa imeanzisha vita vya kisaikolojia dhidi ya Iran kwa kutumua meli na zana zake za kivita katika eneo.