Rais Rouhani: Taifa la Iran litamfanya adui ajute
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: "Kwa mara nyingine, taifa la Iran litamfanya adui ajute katika vita vya kiuchumi."
Rais Rouhani ameyasema hayo Alhamisi usiku katika Kongamano la 12 la Kitaifa la Kuwaenzi Maveterani wa Kivita na kuongeza kuwa: "Taifa la Iran limesimama kidete mbele ya maadui kwa izza." Rais wa Iran ameendelea kusema maadui wamezidisha mashinikizo ili taifa la Iran lisalimu amri lakini taifa la Iran limeonyesha kuwa, njama za maadui hazitazaa matunda na kwa mara nyingine taifa hili litamfanya adui ajute.
Rais Rouhani amebaini kuwa, kwa zaidi ya mwaka moja sasa, pamoja na kuwepo vikwazo na mashinikizo mengi wananchi wa Iran hawajasalimu amri bali wamepaza sauti ya mapambano na muqawama na kusimama kidete. Aidha amesema taifa la Iran halitakubali kudhalilika na kwa kujitolea litaweza kupata ushindi mbele ya maadui.
Rais Rouhani amesema leo kwa kusimama kidete na kwa mapambano sambamba na umoja, taifa la Iran linaweza kushinda katika makabiliaono na Marekani, utawala wa Kizayuni na vibaraka wao katika eneo.
Rais wa Iran amesisitiza kuwa, mji wa Khorramshahr ni nembo ya Kujihami Kutakatifu na ni kielelezo cha izza ya taifa la Iran. Amesema ushindi katika Khorramshahr ulipatikana kwa kushikiliwa mateka maafisa wa kijeshi na askari 19 elfu wa Iraq.
Leo Ijumaa tarehe 3 Khordad sawa na Mei 24 ni siku ya kuadhimisha kukombolewa mji wa Khorramshahr katika mkoa wa Khuzestan kusini magharibi mwa Iran mwaka 1982. Mji wa Khorramshar ulikombolewa baada ya kukaliwa kwa mabavu kwa muda wa siku 578 na jeshi la utawala wa Kibaath uliokuwa ukitawala Iraq wakati huo.