Rouhani: Mapambano ndiyo njia pekee ya kuwakabili wavamizi
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kuwanyooshea mkono wa pongezi wananchi wa Lebanon kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kukombolewa maeneo ya kusini mwa nchi hiyo ya Kiarabu kutoka kwenye makucha ya utawala wa Kizayuni wa Israel, amesisitiza kuwa muqawama ndiyo njia pekee ya kukabiliana na wavamizi.
Katika ujumbe wake kwa Rais Michel Aoun na taifa la Lebanon kwa ujumla kwa mnasaba wa kukumbuka ushindi huo wa mwaka 2000 dhidi ya utawala ghasibu wa Israel, Rais Rouhani amesema historia inaonyesha kuwa, hulka ya uvamizi ya utawala wa Kizayuni haiwezi kuzimwa isipokuwa kwa njia ya mapambano.
Dakta Rouhani amebainisha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kusimama na jeshi na taifa la Lebanon kwa ujumla, katika jitihada za kuimarisha umoja na kuilinda nchi hiyo ya Kiarabu.
Mei 25 mwaka 2000, wanamapambano wa Kiislamu wa Hizbullah ya Lebanon waliwafurusha wanajeshi wa Israel kutoka maeneo ya kusini mwa nchi, na siku hii inatambuliwa nchini humo kama Siku ya Mapambano na Ukombozi.
Kadhalika katika ujumbe wake huo wa pongezi, Rais wa Iran amewatakia kheri, fanaka na afya njema wananchi wa Lebanon.
Itakumbukwa kuwa, utawala haramu wa Israel umekuwa ukianzisha uvamizi na vita vya mara kwa mara vikiwemo vile vya mwaka 2000 na 2006 dhidi ya Lebanon.
Hata hivyo utawala huo pandikizi umekuwa ukipata vipigo vikali kutoka kwa wanamapambano wa Kiislamu wa Hizbullah ya Lebanon.