Japan: Mazungumzo ya Abe Shinzō na Rais Hassan Rouhani, yalikuwa chanya
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Japan ameyataja mazungumzo ya Rais Hassan Rouhani wa Iran na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Abe Shinzō kuwa yalikuwa chanya na yenye faida.
Takeshi Osuga ameyasema hayo asubuhi ya leo mjini Tehran. Akizungumzia baadhi ya habari kwamba imepangwa Abe kumualika Rais wa Iran ashiriki katika kikao cha G20 na kando na mkutano huo aweze kukutana moja kwa moja na Rais Donald Trump wa Marekani, amebainisha kuwa binafsi hana taarifa hiyo na kwamba ni jambo lililombali.
Akiashiria kuwa majina ya nchi zitakazoshiriki kwenye mkutano wa G20 yanajulikana, huku zikiwa zimesalia karibu siku 20 kabla ya kufanyika mkutano huo, amesema kuwa, orodha ya mwisho ya washiriki tayari imekamilika na hadhani kuwa Iran inaweza kuwa katika orodha hiyo.
Wakati huo huo safari ya Waziri Mkuu wa Japan Abe Shinzō nchini Iran imeakisiwa sana na vyombo mbalimbali vya habari vya dunia.

Katika uwanja huo Televisheni ya Taifa ya Japan ya (NHK) leo imetoa ripoti ambayo sambamba na kuakisi safari hiyo imesema kuwa, ziara ya Abe nchini Iran itapelekea kupanuliwa urafiki wa muda mrefu kati ya Tokyo na Tehran. Kadhalika televisheni hiyo ikiashiria kuwa safari hiyo imefanyika kufuatia ongezeko la mizozo katika eneo la Asia Magharibi iliyotokana na tofauti baina ya Iran na Marekani na kwamba Abe ni Waziri Mkuu wa kwanza wa Japan kuitembelea Iran katika kipindi cha miaka 41 iliyopita.
Kwa mujibu wa kanali hiyo ya televisheni ya Japan, amani na usalama wa eneo la Asia Magharibi ni mambo muhimu kwa Japan ambayo inadhamini mahitaji yake yake ya nishati kutoka eneo hilo. Nalo Shirika la Habari la Kyodo la Japan limeashiria safari ya Abe Shinzō nchini Iran ambapo jana alikutana na Rais Hassan Rouhani wa Iran, mkutano wao na waandishi wa habari na mazungumzo yao na kuongeza kuwa katika mazungumzo hayo viongozi hao walizungumzia njia za kupunguza mzozo katika kanda hiyo.