Uhispania: Iran haijavunja hata mara moja mapatano ya JCPOA
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania ambaye anatarajiwa kuchukua nafasi ya Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesisitiza kuwa, uamuzi wa hivi karibuni wa Iran haujavunja vipengee vya mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kimsingi hilo ni suala la kiufundi.
Shirika la habari la IRIB limeripoti habari hiyo na kumnukuu Josep Borrell akisema kwenye mahojiano na redio maarufu ya Uhispania ya Cadena SER kwamba, nchi za Ulaya zinafanya juhudi zao zote kuhakikisha kuwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA yanalindwa na kwa mara nyingine amesisitiza kuwa Iran haijavunja hata mara moja mapatano hayo.
Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Uhispania amesisitiza pia kuwa, kitendo cha rais wa Marekani, Donald Trump, cha kuitoa nchi yake katika mapatano ya JCPOA, kimsingi ndiyo hatua pekee ya kuvunja makubaliano hayo ya kimataifa.
Amma kuhusu uwezekano wa kutokea mapigano ya kijeshi baina ya Iran na Marekani amesema, tunaamini kuwa hatutofika huko, hali haitokuwa mbaya zaidi ya ilivyo hivi sasa na mwisho akili, mantiki na busara zitatumika kuepusha kitu kama hicho.
Siku ya Jumatatu ya tarehe Mosi Julai, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitangaza kuwa imetumia kipengee cha 36 cha mapatano ya nyuklia ya JCPOA kuzalisha urani iliyorutubishwa kwa zaidi ya kilo 300 ikiwa ni kujibu hatua za nchi za Ulaya za kutotekeleza ahadi zao.
Iran inazitaka nchi za Ulaya zitekeleze ahadi zao kwa mujibu wa mapatano ya JCPOA hasa katika masuala ya benki na mafuta vinginevyo hakutakuwa na haja kwa Tehran kuheshimu peke yake vipengee vya makubaliano hayo.