Bunge la Iran laipongeza IRGC kwa kusimamisha meli ya mafuta ya Uingereza
Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) imelishukuru na kulipongeza Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kwa kusimamisha meli ya mafuta ya Uingereza ya "Stena Impero" baada ya meli hiyo kujaribu kupita kwenye Lango Bahari la Hormuz bila ya kuheshimu sheria za kimataifa.
Kufikia Jumapili adhuhuri, wabunge 160 wa Iran walikuwa wamesaini tangazo la kuipongeza SEPAH kwa kuisimamisha meli hiyo ya mafuta ya Uingereza.
Wabunge hao wamesema kitendo hicho cha kikosi maalumu cha Jeshi la Majini la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) ni cha kishujaa na kinachopaswa kupongezwa, haswa kwa kuzingatia kuwa, njama mbalimbali zimekuwa zikipikwa katika wiki za hivi karibuni katika Ghuba ya Uajemi.
Wakati huohuo, Spika wa Bunge la Iran, Ali Larijani sambamba na kupongeza hatua hiyo ya IRGC, amesema, "Waingereza walifanya wizi na uharamia dhidi ya Iran, na Iran imewapa jibu walilostahiki."
Meli hiyo ya mafuta ilikuwa inasindikizwa na meli nyingine ya kivita ya Uingereza na ilijaribu kukizuia kikosi maalumu cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH kuisimamisha meli hiyo ya mafuta lakini ilishindwa.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekanusha vikali madai ya kipropaganda ya vyombo vya habari vya Magharibi kwamba Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran limezuia meli ya pili ya mafuta ya Uingereza katika Ghuba ya Uajemi.
Kwa zaidi ya wiki mbili sasa, Uingereza imeendelea kuizuilia meli ya mafuta ya Iran ya "Grace 1" yenye mapipa milioni 2.1 ya mafuta, iliyosimamishwa na jeshi la majini la UK katika Lango Bahari la Jabal Twariq (Gibraltar).