Araqchi: Kikao cha kamisheni ya JCPOA kimekuwa na mafanikio
Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema kuwa kikao cha kamisheni ya pamoja ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kilichofanyika jana mjini Vienna kimemalizika kwa mafanikio japo hatuwezi kusema kuwa mambo yote yametatuliwa.
Sayyid Abbas Araqchi alisema jana baada ya kumalizika kikao cha dharura cha kamisheni ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA mjini Vienna kwamba: Hatua ya Uingereza na kukamata meli inayobeba mafuta ya Iran katika maji ya Jabal Tariq (Gibraltar) ni ukiukaji wa makubaliano ya JCPOA lakini mazungumzo juu ya kadhia hiyo pia yamekuwa na mafanikio.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: Hatuwezi kusema kuwa mambo yote yametatuliwa lakini tunaweza kusema kwamba, kumetolewa ahadi nyingi katika kikao cha Vienna.
Sayyid Abbas Araqchi ameongeza kuwa, Iran utaendelea kupunguza utekelezaji wa majukumu yake katika makubaliano hayo hadi pale maslahi yake yatakapodhaminiwa.
Baada ya mazungumzo ya kamisheni ya JCPOA, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Mkuu wa Sera za Kigeni za Umoja wa Ulaya, Helga Maria Schmid na vilevile wawakilishi wa Russia na China.
Kikao cha dharura cha kamisheni ya pamoja ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kilifanyika jana kikihudhuriwa na Manaibu Mawaziri na Wakurugenzi wa Kisiasa wa Iran na nchi wanachama wa kundi la 4+1 ambazo ni Ujerumani, Uingereza, Ufaransa, China na Russia. Kikao hicho kimeongozwa na Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran, Sayyid Abbas Araqchi na Naibu Mkuu wa Sera za Kigeni za Umoja wa Ulaya, Helga Maria Schmid.