Kampeni za duru ya pili ya uchaguzi wa bunge Iran zaanza
Kampeni za duru ya pili ya uchaguzi wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran itakayofanyika Aprili 29, zimeanza rasmi hii leo Alkhamisi.
Wagombea 136 watachuana kuwania viti 68 kati ya 290 vya Bunge hilo katika duru hii ya pili ya uchaguzi. Hakuna mgombea yeyote aliyepata idadi ya kura zinazotakiwa katika uchaguzi wa bunge wa Februari mwaka huu katika maeneo-bunge 68.
Muhammad Hussein Muqimi, Mkuu wa Tume ya Uchaguzi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran amesema kuna vituo 15,350 vya kupigia kura katika miji 55 kwenye mikoa 21 ya Iran.
Amesema tayari masanduku milioni 19 yametayarishwa na kupelekwa katika mikoa hiyo kwa ajili ya zoezi hilo.
Imearifiwa kuwa, mrengo wa wapenda mageuzi ya haraka (reformists) umesimamisha wagombea 58 na waliosalia wanatoka katika mirengo mingine huku baadhi yao wakiwa wagombea binafsi.
Itakumbukwa kuwa, asilimia 62 ya wananchi milioni 55 waliotimiza masharti ya kupiga kura walishiriki katika uchaguzi huo wa Bunge la 10 la Jamhuri ya Kiislamu na wa uchaguzi wa tano wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu uliofanyika Februari 26 mwaka huu.