Majeshi ya Iran yako tayari kukabiliana na maadui
Naibu Kamanda Mkuu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema majeshi yote ya Iran yako katika hali ya juu ya utayarifu wa kukabiliana na maadui.
Akizungumza Jumatano mjini Tehran, Brigedia Jenerali Mohammad Hossein Dadras Naibu Kamanda Mkuu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu amesema: "Majeshi ya Iran yako katika hali ya juu ya utayarifu kwa mtazamo wa ulinzi wa angani, nchi kavu na baharini."
Brigedia Jenerali Dadras amesema kuwa, maadui wa Iran wanapinga kuimarika uwezo wa kujihami Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lakini amesisitiza kuwa: "Iran itaendelea kujiimarisha katika sekta za ulinzi."
Naibu Kamanda Mkuu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha ameashiria jinai zinazofanywa maadui na kusema: "Fahari ya maadui ni kuwaua watoto, kutungua ndege za abiria, kuwawekea wananchi vikwazo vya dawa na kubadilisha hafla za harusi kuwa maombolezo huko Afghanistan na Pakistan.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, mnamo Agosti 31 2016, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei, katika mkutano na maafisa wa sekta ya ulinzi alisema kuimarisha uwezo wa kujihami na kuhujumu ni haki ya kimsingi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema katika ulimwengu ambao madola makubwa yanatumia mabavu na hayazingatii maadili huku yakiwaua raia wasio na hatia, kustawisha viwanda vya kuunda zana za kijeshi ni jambo linalotarajiwa, kwa sababu iwapo madola hayo hayatahisi kuwa Iran ina uwezo mkubwa basi hakutakuwa na usalama.