Salehi: Iran inaendelea na miradi yake ya nyuklia kwa nguvu zake zote
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i55673-salehi_iran_inaendelea_na_miradi_yake_ya_nyuklia_kwa_nguvu_zake_zote
Mkuu wa Taasisi ya Nyuklia ya Iran amesema kuwa, shughuli za nyuklia za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zinaendelea kwa nguvu zote katika vitengo vyake vyote na kwamba miradi ya nyuklia ya Iran haijawahi kusimamishwa hata mara moja.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 29, 2019 07:45 UTC
  • Salehi: Iran inaendelea na miradi yake ya nyuklia kwa nguvu zake zote

Mkuu wa Taasisi ya Nyuklia ya Iran amesema kuwa, shughuli za nyuklia za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zinaendelea kwa nguvu zote katika vitengo vyake vyote na kwamba miradi ya nyuklia ya Iran haijawahi kusimamishwa hata mara moja.

Dk Ali Akbar Salehi amesema hayo leo katika sherehe maalumu mkoani Alborz, magharibi mwa Tehran na kuongeza kuwa, kuendelea shughuli za nyuklia za Iran tena kwa nguvu zote ndiko kulikomfanya rais wa Marekani, Donald Trump aseme kuwa, mapatano ya nyuklia ya JCPOA ni makubaliano mabaya zaidi katika historia ya Marekani.

 

Mkuu huyo wa Taasisi ya Nyuklia ya Iran amegusia nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulimwenguni na kusema, eneo la Mashariki ya Kati haliwezi kuwa na sura yake halisi na ya kawaida bila ya kupenda na kuhusika Iran na kwamba Tehran ni moja ya waamuzi wa hali ya hivi sasa na ya baadaye ya Mashariki ya Kati.

Vile vile amesema, changamoto ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na dunia inatokana na ukweli kwamba Mapinduzi ya Kiislamu ni kizuizi kikubwa mbele ya fikra za kiistikbari na kibeberu, na yameyaandalia mataifa ya dunia uwanja wa kuamka na kusimama imara kutetea haki zao.