Iran: Hatufanyi mazungumzo na Marekani iwapo wanaendeleza ugaidi wa kiuchumi
Mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema ni jambo lisilowezekana kwa Jamhuri ya Kiislamu kufanya mazungumzo na Marekani madhali serikali ya Washington inaendeleza ugaidi wa kiuchumi na kuliwekea vikwazo taifa hili.
Majid Takht Ravanchi ameeleza bayana kuwa, Tehran imekuwa ikikariri mara kwa mara kuwa haipo tayari kufanya mazungumzo na Marekani na kwamba jambo hilo linawezekana tu iwapo utawala wa Washington utaliondolea taifa hili vikwazo vyake vya kidhalimu.
Hapo jana, Waziri wa Fedha wa Marekani Steven Mnuchin alidai kuwa Rais Donald Trump yuko tayari kukutana na Rais Hassan Rouhani mwishoni mwa mwezi huu bila masharti yoyote, katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York.
Mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, "Tunaweza kufanya mazungumzo na Marekani iwapo itawaondolewa Wairani vikwazo vya kidhalimu. Na hilo linayumkinika tu katika fremu ya Kundi la 5+1, ambalo lilijadili na kufikia makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015."
Kuhusu hatua ya Trump ya kumpiga kalamu nyekundu Mshauri wa Usalama wa Taifa wa White House, John Robert Bolton, Majid Takht Ravanchi amebainisha kuwa, kadhia hiyo ni ya ndani ya Marekani na Tehran haina cha kusema kuhusu suala hilo.
Wakati huohuo, Abbas Mousavi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran akijibu swali la mwanadishi wa habari juu ya kutimuliwa Bolton, amemnukuu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif ambaye amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu haitatoa taarifa yoyote kuhusu masuala ya ndani ya Marekani.