Iran: Tumevishinda vikwazo vya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i56496-iran_tumevishinda_vikwazo_vya_marekani
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, taifa la Iran limefanikiwa kuvuka kipindi kigumu cha vikwazo na kusema kuwa, licha ya Marekani kuweka vikwazo vikubwa vya kiuchumi, lakini uchumi wa Iran unazidi kuimarika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 08, 2019 08:08 UTC
  • Iran: Tumevishinda vikwazo vya Marekani

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, taifa la Iran limefanikiwa kuvuka kipindi kigumu cha vikwazo na kusema kuwa, licha ya Marekani kuweka vikwazo vikubwa vya kiuchumi, lakini uchumi wa Iran unazidi kuimarika.

Is'haq Jahan-giri amesema hayo katika sherehe za Siku ya Kimataifa ya Viwango na kuongeza kuwa, licha ya Marekani kuiwekea vikwazo vikali Iran, lakini uchumi wa taifa hili unazidi kustawi na kuwa imara.

Ameongeza kuwa dalili na ripoti za kuaminika zinaonesha kuwa uchumi Iran unazidi kukuwa na kuimarika licha ya adui Mmarekani kuweka vikwazo ambavyo anaviita ni vya kiwango cha juu kabisa.

Ameongeza kuwa, adui alidhani kwamba kwa vikwazo vyake hivyo angeliweza kusambaratisha uchumi wa Iran lakini wananchi wa taifa hili wamevuuka kipindi hicho kigumu na uchumi wa nchi yao unazidi kuimarika na kuelekea kwenye kuzalisha nafasi zaidi za ajira, uzalishaji wa bidhaa na ustawi.

Taifa la Iran limesambaratisha vikwazo vya Marekani

 

Itakumbukwa kuwa tarehe 8 Mei 2018, rais wa Marekani, Donald Trump alitangaza kujitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA yaliyokuwa yamefikiwa kati ya Iran na kundi la 5+1 lililokuwa limeundwa na nchi kubwa za dunia ambazo ni Russia, China, Uingereza, Marekani, Ufaransa na Ujerumani. 

Baada ya kujitoa kwenye mapatano hayo, Marekani iliirejeshea Iran vikwazo vyote vilivyokuwa vimeondolewa baada ya kufikiwa makubaliano hayo huku Donald Trump akijitapa kwamba ameiwekea Iran vikwazo vya kiwango cha juu mno. Alijigamba pia kuwa eti atafikisha kwenye sifuri uuzaji wa mafuta ya Iran. Lakini ubeberu wote huo wa Marekani umegonga mwamba mbele ya muqawama wa taifa la Kiislamu la Iran.