Iran: Kuzinduliwa ndege mpya ya kivita ya Yasin, ishara ya kushindwa vikwazo
Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hatua ya Iran kuzindua ndege mpya ya kivita iliyotengenezwa na wataalamu wa kijeshi wa hapa nchini ni ishara tosha kuwa vikwazo vya kidhalimu vya Marekani havijakuwa na athari zozote kwa taifa hili.
Brigedia Jenerali Amir Hatami amesema hayo leo Alkhamisi wakati wa uzinduzi wa ndege hiyo ya kivita kwa jina 'Yasin' katika uwanja wa ndege wa kijeshi wa Noje ulioko katika mkoa wa Hamadan.
Brigedia Jenerali Hatami ameeleza bayana kuwa, "Ndege hii ya kivita imeundwa na wataalamu wa hapa nchini na kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu, jambo ambalo linatuma ujumbe wa wazi kwa madola ya kibeberu kwamba vikwazo vimeshindwa kufikia malengo yake na havijakuwa na athari zilizokusudiwa dhidi taifa la Iran."
Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, ndege ya kivita ya Yasin imeundwa kwa kutumia vipura na vifaa vya hapa nchini, ikiwa ni katika kutekeleza muongozo wa Kiongozi Muadhamu wa kuimarisha uzalishaji wa hapa nchini na kuinua uchumi wa kimuqawama.
Mwezi Mei 2018, Rais Donald Trump aliitoa Marekani kwenye mapatano ya kimataifa ya JCPOA bila ya sababu yoyote ya msingi na tangu wakati huo ameiwekea vikwazo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambavyo mwenyewe anajigamba kuwa ni vikubwa na vikali zaidi kuwahi kuwekwa dhidi ya nchi yoyote ile duniani.
Kujibu uvunjaji huo wa mapatano ya nyuklia ya JCPOA, Tehran nayo ilitoa fursa ya mwaka mzima kwa nchi za Ulaya kuheshimu kivitendo makubaliano hayo, lakini zimeshindwa, hivyo Tehran nayo imeamua kupunguza hatua kwa hatua ahadi zake ndani ya JCPOA hadi pale nchi za Ulaya zitakapoheshimu kivitendo vipengee vyote vya makubaliano hayo.