Raisi: Marekani ifikishwe kizimbani kwa kuasisi kundi la kigaidi la ISIS
Mkuu wa Vyombo vya Mahakama vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: "Marekani imekiri rasmi kuwa ilianzisha kundi la kigaidi la ISIS (Daesh) na kwa msingi huo inapaswa kufikishwa kizimbani kujibu mashtaka kuhusu jinai za kundi hilo."
Sayyid Ibrahim Raisi, Mkuu wa Vyombo vya Mahakama vya Iran ameyasema hayo Jumapili na kuongeza kuwa Marekani ndiye muasisi na muungaji mkono mkuu wa ugaidi duniani. Ameongeza kuwa wataalamu wa sheria duniani, na watetezi huru wa haki za binadamu wanapaswa kutoa mashinikizo ili wanaokiuka haki za binadamu wafikishwe kizimbani.
Mkuu wa Vyombo vya Mahakama Iran ameendelea kusema: "Mienendo iliyo dhidi ya haki za binadamu ya Marekani ikiwa ni pamoja na ubaguzi mkubwa wa rangi, kutungua ndege ya abiria ya Iran, kuwaua watu wasio na hatia Palestina pamoja na Yemen ni jinai ambazo zinapaswa kufuatiliwa katika mahakama za kimataifa."
Ayatullah Raisi amebaini kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatetea haki za binadamu na kuongeza kuwa: "Haki za binadamu ni fursa nzuri ya kuwaonyesha walimwengu utendaji kazi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kutetea haki za binadamu."