Vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Iran; jitihada zilizofeli za Washington
Serikali ya Trump inatekeleza vikwazo dhidi ya Iran ambavyo havijawahi kushuhudiwa huko nyuma baada ya Marekani kujitoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA mwezi Mei mwaka jana 2018 katika fremu ya siasa zake za mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya nchi hii; na ingali inaiwekea Iran vikwazo vipya.
Wizara ya Fedha ya Marekani katika fremu ya siasa za uhasama za Washington dhidi ya Tehran, jana Jumatatu ililiweka katika faharasa ya shakhsiya na taasisi zinazokabiliwa na vikwazo vyake jina la taasisi moja na maafisa tisa wa serikali ya Iran. Wizara hiyo imetangaza kujumuishwa jina la Kamandi ya Majeshi yote ya Iran na vile vile majina ya shakhsiya tisa wa Iran akiwemo Sayyid Ibrahim Raisi, Mkuu wa Vyombo vya Mahakama vya Iran, Brigedia Jenerali Muhammad Baqeri Mkuu wa Kamandi ya Majeshi yote ya Iran na pia maafisa kadhaa wa Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika orodha ya shakhsia na taasisi zilizo chini ya vikwazo vya Washington. Wizara ya Fedha ya Marekani imeashiria katika taarifa yake iliyoitoa jana sambamba na maadhimisho ya kutekwa pango la ujasusi la nchi hiyo hapa Tehran yaliyofanyika kote hapa nchini kuhusu tukio hilo nyeti la kuiwekea vikwazo Kamandi ya Majeshi ya Iran na maafisa tisa wa nchi hii ambao wametajwa kuwa maafisa wa ngazi ya juu wa serikali; na kusema hatua hiyo imechukuliwa ili kukabiliana na uwezo wa ndani na wa kieneo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Serikali ya Trump hivi sasa inatekeleza vikwazo vikali dhidi ya Iran ambavyo havijawahi kushuhudiwa baada ya Marekani kujitoa kwa upande mmoja kwenye makubaliano ya nyuklia mwezi Mei mwaka jana ili kuishinikiza Iran kila upande. Serikali hiyo aidha imewawekea shakhsia na taasisi za Iran vikwazo mbalimbali na wakati huo huo kutumia vitisho dhidi ya nchi nyingine ili ziunge mkono vikwazo vyake hivyo haramu. Hata hivyo, siasa hizo za serikali ya Trump zimekosolewa vikali kimataifa. Lengo la Washington ni kuilazimisha Iran ikubali matakwa yake yaliyo kinyume cha sheria katika kalibu ya masharti 12 yaliyowekwa na Mike Pompeo Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi hiyo mwezi Mei mwaka jana.
Nukta muhimu katika vikwazo vipya vilivyotangazwa na Wizara ya Fedha ya Marekani ni kuwekewa vikwazo viongozi na shakhsia katika Ofisi ya Kiongozi Muadhamu; jambo linaloonyesha pia namna msimamo wa wazi wa Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu wa kupinga kufanya mazungumzo yoyote na Marekani ulivyoikatisha tamaa na kuivunja moyo Washington. Serikali ya Trump ilitaraji kuwa kwa kuzingatia siasa zake za mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya Iran ingeweza kuipigisha magoti nchi hii ili iketi kwenye meza ya mazungumzo sambamba na Tehran kukubali matakwa haramu ya Washington kukiwemo kusitisha miradi yake ya nyuklia na makombora na pia ibadili siasa zake katika eneo. Pamoja na haya yote, msimamo thabiti na wa wazi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu umeibainishia wazi Washington jambo hili kwamba, siasa zake za mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Iran hazitakuwa na natija yoyote ile. Ayatullah Khamenei amesisitiza mara kadhaa kuwa Iran imestafidi na vikwazo hivyo kama fursa kwake na kuboresha uwezo wake wa ndani. Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mwezi Mei mwaka huu aligusia suala hilo akisema: "Vikwazo hivi vimetufanya tujitazame, tuangalie tuzalishe nini ili kujidhaminia mahitaji yetu na kutambua ubunifu wetu."
Suala jingine ni kuwa, Marekani imefikia mwisho katika upande wa vikwazo; na hakuna kingine kilichosalia kuhusu vikwazo hivyo. Mtandao wa Bloomberg umeripoti kuwa: Siasa za kuiwekea vikwazo Iran zimefika mwisho na Marekani sasa haina machaguo mengi kwa ajili ya kuweka vikwazo zaidi. Katika wiki za karibuni ambapo Marekani imeweka vikwazo katika sekta kadhaa kama ile ya ujenzi ambayo ina utegemezi wa kiwango cha chini kwa biashra ya nje; na vile vile kwa baadhi ya shakhsia ambao kwa muda sasa hawana nyadhifa zozote za utendaji; hatua yake hii inaonyesha kuwa ripoti zinazosema kuwa vikwazo vya Marekani vimefikia mwisho zina ukweli. Taasisi za Kimataifa zikiwemo Benki ya Dunia na Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) zimetangaza kupitia ripoti zake za karibuni kwamba taathira za vikwazo kwa uchumi wa Iran zimepungua kwa kiasi fulani na uchumi wa Iran mwaka ujao unaweza kurejea katika hali yake ya kawaida. Wakati huo huo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza mara kadhaa kwamba licha ya vikwazo vyote vya Marekani haitasalimu amri mbele ya matakwa ya uistikbari; na kwa kuzingatia nchi za Ulaya kutochukua hatua kuhusu makubaliano ya JCPOA, Iran hadi sasa imetekeleza kwa mafanikio hatua yake ya tatu ya kupunguza uwajibikaji wake katika fremu ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Aidha inatabiriwa kuwa Iran itachukua hatua ya nne pia ya kupunguza uwajibikaji wake ndani ya JCPOA ifikapo tarehe 6 mwezi huu.