Iran yapinga azimio la haki za binadamu la UN dhidi yake
Iran imepinga azimio dhidi yake kuhusu haki za binadamu ambalo limetolewa na Umoja wa Mataifa na kusema limetokana na utashi wa kisiasa, ni mfano wa unafiki na nchi za Magharibi kutumia vibaya mfumo wa Umoja wa Mataifa kulenga nchi huru na zinazojitegemea.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Abbas Mousavi ametoa kauli hiyo punde baada ya Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio ambalo liliwasilishwa na Canada na ambalo limekosoa rekodi ya haki za binadmau nchini Iran.
Katika upigaji kura wa Alhamisi nchi 182 zilishiriki ambapo nchi 84 ziliunga mkono azimio hilo, 30 zikapinga na 66 zikajizuia kupiga kura.
Katika upigaji kura, Pakistan, Syria, Venezuela na Belarus zilipinga vikali azimio hilo. Aidha China na Russia nazo zilibainisha upinzani wao na kulalamikia kutumiwa kisiasa kadhia ya haki za binadamu nazo Korea Kaskazini na Cuba zimesema azimio hilo ambalo liliwasilishwa na Canada lilikuwa na lengo la kushinikiza na kuvuruga serikali zingine.
Akizungumza baada ya kupigiwa kura azimio hilo, Mousavi amesema baadhi ya nchi ambazo zimeunga mkono azimio hilo zenyewe zina historia ndefu ya ukiukaji wa haki za binadamu. Amesema mmoja wa waungaji mkono azimio hilo ni serikali ya Marekani ambayo inakiuka haki za binadamu za raia milioni 83 wa Iran kupitia ugaidi wa kiuchumi, hasa kwa kuwalenga wanawake, watoto, wazee na wagonjwa.
Aidha amesema baadhi ya waungaji mkono wa azimio hilo kama vile Israel na 'tawala zilizobaki nyuma' katika eneo ni wahusika wakuu katika mauaji ya watu wa Palestina, Yemen na ukandamizaji wa wapinzani ndani ya tawala hizo.